Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Cuba yaridhia kuipa Tanzania chanjo ya COVID-19

DSYRY Serikali ya Cuba yaridhia kuipa Tanzania chanjo ya COVID-19

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: Habarileo

SERIKALI ya Cuba imesema iko tayari kutoa ushirikiano, uzoefu, ushauri na kuisaidia Tanzania kutengeneza chanjo ya ugonjwa wa Covid-19.

Balozi wa Cuba nchini, Profesa Lucas Polledo, alisema hayo nyumbani kwake Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa kampuni ya magazeti ya serikali (TSN).

Profesa Polledo alisema Cuba imetengeneza chanjo tano za Covid-19, mamlaka za ndani zimezithibitisha tatu zitumike na asilimia 89.9 ya raia wa nchi hiyo wamechanjwa dozi milioni 26.

Alitaja chanjo hizo kuwa ni Soberana 02 na Abdala ambazo ni kwa ajili ya kuwachanja watu wote na chanjo ya Soberana Plus ni maalumu kwa matumizi ya nchini humo kuwachanja waliombukizwa Covid-19 na wakapona.

Alisema chanjo ya Abdala na Soberana 02 wameziombea usajili kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) ili zitambulike kimataifa.

“Nchi kujitengenezea chanjo yenyewe ni jambo jema sana. Asilimia 100 kwa 100 Tanzania inaweza, kama itapenda, kupata ushauri kutoka Cuba kwa sababu Cuba ina uzoefu wa kutengeneza chanjo. Chanjo hizi tano ni za kwetu, tumetengeneza wenyewe, mbili kati ya hizo zinatambulika kwenye taasisi zetu kama chanjo. Sisi mnaotuona hapa tumeshapata chanjo ambazo zimetengenezwa nchini kwetu,” alisema Balozi Polledo.

Alisema chanjo ya Abdala dozi yake ni mara tatu kila baada ya siku 15, Soberana 02 dozi yake ni mara mbili kila baada ya siku 28 na Soberana Plus dozi yake ni mara moja. Alisema Covid-19 imeonesha uwezo na umahiri wa uvumilivu wa Cuba.

“Chanjo yetu ambayo tumetengeneza wenyewe imeokoa maisha ya watu wengi Cuba. Hii chanjo ya Cuba ikipitishwa na WHO kama tunavyotegemea, nchi za Afrika na ndugu zetu wa Afrika kwa ujumla lakini hasa Watanzania, nitawasihi muipokee hii chanjo kwa sababu ni chanjo salama. Hii chanjo imeonesha matokeo na hakuna mjadala wowote umetokea kuhusu chanjo ya Cuba, tunategemea WHO waipitishe kama walivyoipitisha chanjo nyingine,” alisema Profesa Polledo.

Alisema chanjo hizo ni matokea ya kazi ya utafiti uliyofanywa na wataalamu wao watano na wakapata chanjo hizo.

Alisema kuanzia leo Novemba 15 Cuba itarejea katika hali ya kawaida, shule zote zitafunguliwa, mipaka yote ya nchi itafunguliwa, ndege za kimataifa zitaanza tena kutua nchini humo

Chanzo: Habarileo