Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuzingatia mafungu maalum ya fedha wenye VVU

Waziri Jenista Mhagama Serikali kuzingatia mafungu maalum ya fedha wenye VVU

Fri, 26 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amesema utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na vipaombele vingine inazingatia pia mafungu ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) katika kila Wizara na Taasisi.

Ameyasema hayo jana Jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA).

Waziri Mhagama alisema kuwa hii ni namna ambavyo Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kwa dhati kusaidia utekelezaji wa Afua za masuala ya UKIMWI nchini, kwa kuzingatia maeneo muhimu ikiwemo masuala ya lishe bora, dawa za kupunguza makali ya virusi na kuhakikisha mambo mengine yanayochangia ustawi wao kupatikana.

Akizungumzia suala la Sera ya Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001 Waziri Mhagama alisema kuwa kuna kila Sababu ya Sera hiyo kufanyiwa mapitio na maboresho kwani ni ya muda mrefu na kuona, namna gani sekta zote zinaweza kushiriki katika suala hili ili kuweza kuyafikia malengo ya dunia ya kupunguza vifo, maambukizi na unyanyapaa ifikikapo 2030.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa NACOPHA Mwalimu Leticia Mourice ameishukuru Serikali kwa juhudi zake katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live