Dar es Salaam. Serikali imetangaza ajira za madaktari 1,000 ili kujaza nafasi mbalimbali katika hospitali zote kuu, za halmashauri, za rufaa za mikoa na vituo vya afya.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi na nyingine ya Wizara ya afya, jana zilieleza kuwa madaktari hao wametakiwa kuanza kufanya maombi ya ajira hizo kuanzia jana Machi 24 hadi Aprili 10, mwaka huu.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu ajira hizo Katibu Mkuu wa Tamisemi, Joseph Nyamuhanga alisema ni ahadi ya ajira za wataalamu wa afya iliyotolewa na Rais John Magufuli Februari 20, mwaka huu katika mkutano wa madaktari na watumishi wa sekta ya afya uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Madaktari wanaotakiwa kuwasilisha maombi hayo ya ajira ni waliohitimu vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vinavyotambulika na Serikali, waliomaliza mafunzo ya kazi kwa vitendo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na kupata usajili kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika.
Wengine ni wasiokuwa waajiriwa wa Serikali na hospitali za mashirika ya dini ambao mshahara wao wanalipwa na Serikali, ambao hawajawahi kuajiriwa serikalini na wasiokuwa na cheki namba.
Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu uamuzi huo wa Serikali, Rais wa Chama cha Madaktari nchini (MAT), Dk Elisha Osati alisema, “Rais ametimiza ahadi ambayo alituahidi, naweza kusema ahadi imetimizwa.”
Habari zinazohusiana na hii
Katika mkutano huo na madaktari, Rais Magufuli alitoa kibali cha ajira hizo ili kutatua changamoto ya uhaba wa wataalam wa afya na akabainisha kuwa madaktari karibia 2,700 hawajaajiriwa. Alipoulizwa ajira hizo zitapunguza kwa kiasi gani pengo la uhaba wa madaktari nchini na iwapo watatumika katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, Nyamuhanga alisema wengine wataajiriwa na wizara ya afya.
“Katika tangazo letu tumesema ambao watakuwa wameomba kupitia wizara ya afya wasiombe (kupitia halmashauri).”
Alisema madaktari hao wataimarisha mapambano dhidi ya corona ingawa kibali kilitolewa na rais kabla ya tatizo hili kuwa kubwa.
“Itasaidia kupunguza uhaba wa madaktari hata katika mapambano ya virusi hivyo,” aliongeza.
Alipoulizwa mahitaji ya madaktari yaliyopo kwa sasa alisema, “siwezi kusema moja kwa moja ila itasaidia sana. Zamani tulikuwa tunachanganya ajira za watumishi wa sekta ya afya ila kwa sasa tunaajiri madaktari tu kwa hiyo itapunguza sana.”
Katibu Mkuu wa Wizaya Afya, Zainab Chaura alisema wizara hiyo pia imetangaza nafasi 390 kwa ajili ya madaktari kwenye hospitali zilizo chini yake.
Hospitali wanakopelekwa madaktari waliotangazwa na wizara hiyo, ni 306 wa hospitali za rufaa za mikoa, Muhimbili (40), Benjamin Mkapa (20), Taasisi ya Mifupa Moi (10) JKCI (7) na Ocean Road saba.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tamisemi, madaktari wanaotakiwa ni wa daraja la pili, madaktari wa meno daraja la pili na waombaji wawe na shahada ya udaktari wa binadamu au meno.”
Sifa nyingine ni wawe na umri usiozidi miaka 45 huku wakitakiwa kuainisha mikoa mitatu ambayo wangependa kupangiwa kufanya kazi. “Waombaji wote wawe tayari kufanya kazi na mashirika, taasisi zilizoingia ubia na Serikali.”
Inaeleza kuwa waombaji wanatakiwa kuwasilisha maombi kwa njia ya kielekroniki na kuwa watakaowasilisha kwa njia ya posta au kupeleka moja kwa moja maombi yao hayatafanyiwa kazi.