Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuongeza hospitali nyingine ya moyo

Moyo Cardiac Serikali kuongeza hospitali nyingine ya moyo

Tue, 7 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema itajenga hospitali ya moyo katika kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam ili kukiimarisha Kituo cha Afrika Mashariki cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema hayo jana kwenye kampasi hiyo wakati akizindua kituo hicho cha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).

Alisema magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka na kuwa tishio duniani na kama hatua za makusudi hazitachukuliwa yataendelea kupoteza uhai wa watu wengi.

Akitoa mfano wa namna magonjwa yasiyoambukiza yanavyoua watu wengi, Othman alisema kwa nchi za EAC asilimia 35 ya vifo vinatokana na maradhi hayo.

Kwa Tanzania pekee alisema asilimia 33 ya vifo vyote nchini vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza na nusu ya hiyo asilimia ni vifo vya magonjwa ya moyo.

Alisema ujenzi wa hospitali hiyo ya moyo utakamilisha upatikanaji wa huduma za mafunzo kwa vitendo na tiba kituoni hapo.

"Tuna uhaba wa wataalamu wa tiba hapa nchini na ujenzi wa kituo hiki kitatumika kufundishia wanachuo wanaosoma udaktari wa moyo na mishipa ya moyo ambao wataongeza idadi ya wataalamu bingwa wa eneo hilo," alisema Othman.

Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema ujenzi wa kituo hicho umegharimu Sh bilioni 21.7 fedha ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Alisema Sh bilioni tisa kati ya fedha hizo zimetumika kununua vifaa vitakavyotumika katika kituo hicho na pia zimetumika kwa ajili ya mafunzo ya wakufunzi.

Alisema serikali inatambua umuhimu wa kituo hicho na serikali ipo kwenye mazungumzo na AfDB ili isaidie pia awamu ya pili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Mwenyekiti wa Baraza la Muhas, Dk Harrison Mwakyembe alisema kituo hicho cha umahiri ni wazo la serikali la miaka zaidi ya 10 iliyopita.

Alisema serikali ya Tanzania na serikali za EAC zilikubaliana kila nchi ianzishe kituo cha umahiri katika eneo moja na Tanzania ikajenga kituo hicho cha moyo.

Alisema Kenya wamejenga kituo cha umahiri cha figo na hospitali kubwa vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 42.55

Alisema Uganda wamejenga kituo cha umahiri cha saratani kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 38.28, Rwanda wamejenga cha uhandishi na Tehama kwa Dola za Marekani milioni 19 na Burundi wamejenga chuo cha sayansi ya lishe kwa dola za Marekani milioni 18.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live