Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuongeza hatua za mapambano dhidi ya UKIMWI

HIVAIDS Ribbon 1600x900.png Serikali kuongeza hatua za mapambano dhidi ya UKIMWI

Tue, 1 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu ) Balozi Pindi Chana amepongeza Mkoa wa Njombe kwa jitihada za kupunguza viwango vya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Waziri Pindi amesema hayo katika ziara yake Mkoani Njombe alipopokea taarifa ya Mkoa kuhusu utekelezaji wa shughuli za UKIMWI na baadaye kutembelea vikundi vya wajasiriamali vya WAVIU, pamoja na kukagua ujenzi wa Kituo cha Care Treatment Centre (CTC), katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani hapo..

Pindi alisema licha ya kupungua kwa maambukizi hayo bado ipo haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kudhibiti maambukizi mapya na wananchi kuwa katika hali ya usalama na afya bora.

“Nipongeze hatua hii kubwa mliyopiga kama Mkoa lakini tuna jukumu la kuendelea kupunguza viwango hivi na kama Serikali tumefanikiwa kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kina mama pia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” alisema Mhe. Pindi.

Vile vile alibainisha kwamba katika kuhakikisha vikundi vya ujasiriamali vya WAVIU vinaimarika kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali wanazozifanya kuendesha maisha na kupata huduma muhimu serikali imetenga 10% kwa ajili ya Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupata mikopo itakayowawezesha kuboresha shughul zao.

“Mashirikiano ya Serikali za mitaa na vikundi vya wajasiriamali ni imara sana na niwasisitize mtumie fursa hii ya mikopo ambayo inatolewa na serikali yetu lengo ni kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika maendeleo na mtapata na elimu ya matumizi sahihi ya hiyo mikopo na ujasirimali,” alieleza Pindi.

Aidha alihimiza ushirikiano baina ya vikundi vya ujasirimali kushirkiana na serikali za mitaa katika maneo yao ili kupata taarifa za fursa mbalimbali pindi zinapojitokeza katika maeneo yao huku akisisitiza WAVIU kujiunga katika vikundi na kuendelea kuchapa kazi kwa manufaa yao na kuinua pato la Taifa.

Katika hatua nyingine Balozi Pindi alitoa wito kwa wananchi kutumia kituo kinachotoa huduma za afya cha Care Treatment Centre (CTC) kujua hali ya afya zao akisema kuwa suala la kujua hali ya kiafya hususani VVU ni jambo la msingi.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania ( TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko alisema mradi wa Southern Afrika Trade and Transportation Facilitation Project umehusisha ujenzi na ukarabati wa kituo hicho, maabara ya kupima virusi vya ukimwi, kutoa mashine za kupima virusi vya ukimwi na vichomea taka.

“Ujenzi huu pia umehusisha ujenzi wa vituo 20 katika barabara kuu kutoka Dar es salaam kuelekea mpaka wa Tunduma na Kasumulu kwa ufadhili wa World Bank kwa sababu ndio mwingiliano wa Tanzania na Nchi za Jangwa la Sahara ambazo kiwango cha maambukizi kiko juu na vituo hivi vimejengwa katika vituo vya afya na vitakuwa chini ya Halmashauri. ,”alifafanua Dkt. Maboko.

Akitaja mikoa mingine ambayo vituo hivyo vinajengwa ni pamoja na Mkoa wa Pwani wenye vituo vitano vya CTC, Mkoa wa Morogoro vituo vitatu ,Mkoa wa Iringa vituo vinne, Mkoa wa Njombe wenye kituo kimoj pamoja na Mkoa wa Mbeya wenye vituo vitano na Mkoa wa Songwe vituo viwili.

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Jukwaa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Bi, Joseline Mtono ameishukuru Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na kuwajali watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI hali inayowafanya kujisikia nao ni sehemu ya jamii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live