Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuokoa bil 33/- uagizaji dawa, glovu

B1e0f0e15004a856bc92a2523d0960fb.jpeg Serikali kuokoa bil 33/- uagizaji dawa, glovu

Tue, 20 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema viwanda vya dawa na mipira ya mikono (glovu) vilivyopo mkoani Njombe vitaiwezesha serikali kuokoa Sh bilioni 33 ambazo zingetumika kwa mwaka kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.

Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) alieleza kuwa viwanda hivyo vipo Idofi wilayani Makambako.

“Viwanda hivi vinamilikiwa na serikali kupitia Bodi ya Dawa (MSD),” aliandika Msigwa kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter.

Mei 11, mwaka huu wakati ikiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wizara hiyo ililieleza Bunge kuwa MSD ilianzisha kiwanda cha glovu ili kukabili upungufu wa bidhaa hiyo duniani.

Waziri Dk Dorothy Gwajima aliwaeleza wabunge kuwa kiwanda hicho kitakidhi mahitaji ya ndani ya nchi na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Dk Gwajima alisema kiwanda hicho kitaipunguzia serikali mzigo wa fedha za kigeni wastani wa Dola za Marekani milioni 7.9 zinazotumika sasa kwa mwaka kwa ununuzi wa bidhaa hizo.

Alisema bungeni jijini Dodoma MSD ilikuwa katika hatua za mwisho za kuanzisha viwanda vya kuzalisha vidonge, vimiminika na capsules katika eneo la viwanda, Idofi.

“Kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge 24,000,000 kwa siku, sawa na mahitaji ya nchi kwa miezi mitatu. Hivyo, kiwanda hiki kina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya vituo vya afya nchini kwa kuzalisha siku nne tu,” alisema Dk Gwajima.

Alisema kiwanda hicho kitazalisha bidhaa hizo kwa ajili ya mahitaji ya nchi za EAC, SADC na nchi nyingine duniani zitakazohitaji bidhaa hizo.

“Mheshimiwa Spika, ongezeko hili la viwanda vya ndani vya dawa litapunguza kwa kiwango kikubwa gharama ambayo serikali imekuwa ikiingia kwa kuagiza dawa hizi kutoka kwa wazalishaji wa nje, lakini pia itapunguza sana matumizi makubwa ya fedha za kigeni ambazo zimekuwa zikitumika kuagiza dawa hizi nje ya nchi. Vilevile, viwanda hivi vitawezesha upatikanaji wa ajira kwa vijana na wataalamu wengi wa kitanzania”alisema Dk Gwajima.

Chanzo: www.habarileo.co.tz