Utapiamlo sugu au udumavu kwenye baadhi ya jamii unadhoofi sha maendeleo ya uhakika wa chakula, uboreshaji wa elimu na afya bora ya mama na mtoto nchini.
Udumavu huu unachangiwa na upungufu wa ulaji wa vyakula visivyo na virutubishi, ulaji wa ziada ya vyakula vyenye virutubishi. Pia ukosefu wa ulinganifu wa virutubishi kwenye vyakula muhimu au matumizi ya ujali wa vyakula vyenye virutubishi vilivyo na dosari.
Kutokana na changamoto hii, kila mwaka serikali hutumia fedha nyingi kugharamia huduma za afya ili kukabili utapiamlo wa aina zote katika jamii. Kwa mantiki hiyo, suala la kuboresha lishe ni la msingi katika kufanikisha malengo yote ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa jamii na taifa.
Katika kuunga mkono mkakati wa kuboresha lishe, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda anasema utapiamlo unatakiwa kuendelea kupigiwa kelele. Pinda anasema suala la utapiamlo bado ni kubwa nchini na kusababisha udumavu kwa kiwango cha asilimia 31 kwa watu wake.
Anasema haya katika ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro iliyojumuisha mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro.
Pinda anasema suala la lishe bora ni vyema likapigiwa kelele na kuacha kubebeshwa lawama serikali kutokana na watoto wanaozaliw nyakati nyingine kuwa na uzito mdogo. Anasema kwamba wataalamu wamekuwa wakieleza kuwa wajawazito wengi wamekuwa na upungufu wa damu na wanapofikia muda wa kujifungua wanapata matatizo na hiyo ni kutokana na kula vyakula bila kujali lishe bora.
“Mimi natoka Katavi tunatamba kwa kulima mahindi lakini ugali wa mahindi niliozoea ni kwamba ukobolewa ulowekwe kwenye maji wiki moja halafu uanikwe kidogo na kupelekwa kusangwa mashine eti kupata ugali mzuri wa kunukia hii si hoja,” anasema Pinda.
Anasema “Kumekuwa na mazoea kuwa wanaokula dona ni wafungwa pekee na hii si sawa, pale watu wengi wanakula wanga (stach) ndani yake hakuna kitu sasa tuna mtihani mkubwa wa kusemea lishe”. Anasema pamoja na mikoa ya Rukwa na Katavi kuongoza katika kulima mahindi lakini mikoa hiyo ni miongoni mwa mikoa yenye tatizo la utapiamlo.
Pinda anashauri watu wale mbogamboga na vyakula bora ili kupambana na utapiamlo. Anasema ulimwengu unakiri kuwa mboga zenye asili ya Afrika ni bora zaidi kwa lishe. “Nataka tutoke hapa (kwenye maonesho ya Nanenane) kwenda kulima bustani za mboga na si kulima kwa ajili biashara pekee bali kulima kwa kula ili kupata afya bora, hivyo Nanenane kwangu tutumie kujifunza kilimo hicho,”anasema Pinda.
Anawataka wananchi kutumia ufugaji bora ukiwemo wa samaki kwa kutumia njia za kisasa. Anasema sekta ya kilimo bado ni muhimili kwa nchi hivyo kilimo kikitetereka ni sawa na mtu akitetereka na mgongo wake. “Ndiyo maana ipo kauli inayosema kilimo ni uti wa mgongo kwa hiyo kilimo ni muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa letu,” anasema Pinda.
Pinda anasema kutokana na umuhimu wa kilimo, serikali imeongeza mara dufu bajeti ya kilimo katika mwaka wa fedha wa 2022/2023. Katika kuweka mkazo suala la lishe bora hasa kwa watoto, Rais Samia Suluhu Hassan ameligusia alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Mbeya.
Msisitizo wa ufuatiliaji wa huduma za lishe uliuguza mkoa huo lakini agizo la Rais Samia linatosha kuwagusa hata viongozi wa mikoa mingine inayotajwa kuwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula hasa mahindi na bado baadhi ya wananchi wake wanakabiliwa utapiamlo uliokithiri.
Rais Samia alisema Mkoa wa Mbeya unazalisha chakula kingi tena cha kila aina lakini bado katika ripoti yake ya lishe, mikataba yake na wakuu wa mikoa, Mbeya bado haijafanya vizuri. Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu masuala la lishe imeeleza kwamba imedhamiria kukabili changamoto zinazotokana na ukosefu wa lishe bora ambazo ni utapiamlo, udumavu, ukondefu na upungufu wa damu kwa wajawazito na watoto katika jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tanzania imepiga hatua ya kupunguza tatizo la utapiamlo kwa kuzingatia tafiti iliyofanywa mwaka 2018 na 2019. Kwa mujibu wa tafiti hizo kwenye utapiamlo imetoka asilimia 3.8 na kufikia asilimia 3.5 pamoja na kupunguza tatizo la udumavu kutoka asilimia 34 hadi 31. 8.
Mkoa wa Morogoro takwimu zinaonesha hali ya lishe kwa baadhi ya jamii bado ni mbaya. Haya yamebainishwa katika uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya mwaka 2021/2022 -2025/2026 kwa ngazi ya Mkoa wa Morogoro.
Programu hiyo ilizinduliwa Kitaifa Desemba mwaka 2021 jijini Dodoma na mapema mwaka huu mkoani Morogoro. Licha ya kiwango cha utapiamlo na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano kwa mkoa huo kushuka kutoka asilimia 33.4 mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 26.4 mwaka 2018, kiwango hicho kinaonesha tatizo bado ni kubwa.
Naye Mratibu wa Lishe wa mkoa huo, Salome Magembe anasema kushuka kwa asilimia hizo za udumavu kumetokana na serikali kutoa msisitizo katika kuzingatia masuala ya lishe kwa watoto wadogo, wajawazito na walio katika umri wa kuzaa.
“Ukosefu wa lishe kwa mtoto kunachangia kupata udumavu wa aina mbili ukiwemo wa kiakili, unaweza kumwona mtoto mwili wake kuendelea vizuri na hilo linagundulika kutokana na uwezo wake wa kiakili, uwezo wake wa kufikiri unakuwa umepungua na kwa upande wa elimu mtoto aliyeduma hawezi kufundishika,” anasema Magembe.
Hivyo suala la utapiamlo umekuwa na gharama kubwa za kijamii na kiuchumi kwa makundi mbalimbali hususani watoto, wajawazito na wanaonyonyesha, wazee, wagonjwa na wenye kinga dhaifu.
Naye Ofisa Mipango wa Shirika lisilo la Kiserikali la Childhood Development Organisation (CDO), Innocent Rusomyo anasema Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ngazi ya Kitaifa imeteua shirika hilo kuwa kiongozi kiunganishi cha utekelezaji wa mpango huo kwa Mkoa wa Morogoro.
Anasema CDO kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Morogoro na Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN), Shirika la Sawa Wanawake Tanzania na Shirika la Feed the Children wamezindua programu hiyo kwa lengo la kuendelea kutoa elimu ya lishe bora kwenye jamii.