SERIKALI imejipanga kuendelea na kampeni ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo katika mwaka wa fedha 2020/21 itaendelea kujenga hospitali, vituo vya afya pamoja na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini.
Akielezea mipango ya baadaye ya serikali katika kuboresha huduma za afya nchini mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyetembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Uhuru jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga alisema katika kipindi cha mwaka 2020/2021, serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya afya katika maeneo mbalimbali nchini.
Nyamhanga alisema kwa mwaka 2020/2021, serikali imepanga kuendelea na ujenzi wa hospitali za halmashauri 27 ambazo kila moja imetengewa Sh bilioni moja.
Katika mkakati huo huo, pia serikali imetenga Sh bilioni 27.75 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya zahanati katika kila kijiji na maeneo mbalimbali nchini.
Mkakati wa serikali ni kujenga zahanati 555 idadi ambayo inafanya kwamba katika kila halmashauri ya wilaya zitajengwa zahanati tatu.
Katika mkakati huo, kila zahanati moja imetengezwa Sh milioni 50 kwa ajili ya kujenga miundombinu yake hadi kukamilisha na kuanza kutumika kwa ajili ya kusaidia wananchi kupata huduma za afya vijijini mwao.
Kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Uhuru katika wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, Nyamhaga alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa wakati wa maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru mwaka 2018.
Rais Magufuli aliahirisha maadhimisho hayo akaagiza kwamba badala ya Sh milioni 995.1 kutumika kwa ajili ya maadhimisho zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo kubwa kwa ajili ya kutoa huduma ya afya kwa watendaji wa serikali katika mji wa serikali, viongozi na wananchi wa wilaya ya Chamwino na mkoani mzima wa Dodoma.
Pia, Januari 2019, wakati Rais Magufuli akipokea gawio la hisa za kampuni ya simu ya Airtel, aliagiza kwamba Sh bilioni 2.415 zitumike kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo muhimu kwa wananchi wa Dodoma.
Nyamhanga alisema hadi Novemba 19, mwaka huu, Sh bilioni 4.43 zimepokelewa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ambao unaendelea kwa kasi. “Kiasi ambacho kimetumika hadi sasa ni Sh bilioni 4.1 na kiasi ambacho hakijatumika ni sh milioni 368.4”.
Kwa upande wake Mjenzi wa hospitali ya Uhuru, Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali Laurence Lukema alisema watahakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kwa wakati.