Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali imetoa onyo hili kwa wahudumu wa Afya

Mwanaidi.png Naibu waziri wa Afya , Mwanaidi Ali Khamis

Wed, 15 Sep 2021 Chanzo: Channelten

Serikali imesema haitavumilia vitendo vinavyofanywa na wahudumu wa afya kwa kutofuata miongozo na maelekezo ya kutoa huduma bora ya afya kwa wazee kwa kuwa wazee wengi hukutana na manyanyaso na kushindwa kupewa kipaumbele katika huduma za afya.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis mkoani Kagera alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo na kukagua hali ya utoaji huduma ya afya kwa wazee, wanawake na watoto.

Naibu waziri huyo amesema kuhusu suala la maelezo kuhusu baadhi ya dawa kutotolewa kwa wazee kutokana na maelekezo ya Bima ya Afya yanahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Nimeambiwa kwamba baadhi ya dawa hazipatikani kwa wazee kwa maelekezo kadhaa kulingana na viwango na uwezo wa hospitali tusingependa kusikia baadhi ya wazee wanakosa dawa kwa sababu yoyote” amesema

Aidha, Mwanaidi amemuelekeza Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kuwasilisha taarifa ya upatikanaji wa dawa Wizarani ili kuhakikisha wazee na makundi mengine ya kipaumbele yanapata huduma stahiki.

Katika hatua nyingine, Mwanaidi ametembelea wodi ya watoto, wajawazito na wazazi na kupata maelezo ya huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

Aidha, amewapongeza watoa huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuongeza kwamba kazi hiyo ni ya wito hivyo waendelee kujitoa na kufanya kazi kwa moyo.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza Kiilima nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba na kuiagiza Wizara kuendelea kutoa huduma kwa wazee hao.

Chanzo: Channelten