ZAIDI ya Sh bilioni 2.3 zimetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Hatua hii inaelezwa kuwa itasaidia wananchi kupata huduma bora za afya na kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Godwin Chacha, alibainisha hayo wakati akizungumza na HabariLEO jana mjini hapa.
Alisema, tayari serikali imeshatoa fedha hizo kwa awamu tofauti kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo na kwamba, katika awamu ya kwanza, walipokea Sh bilioni 1.5, awamu ya pili Sh milioni 300 na awamu ya tatu Sh milioni 500.
"Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kutuletea fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa fedha ulioisha, kubwa tumepokea shilingi bilioni 2.3 ili kuendelea na ujenzi wa hosptali ya wilaya tunayoijenga eneo la viwanda,” alisema.
Akaongeza: “Ikikamilika, itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wetu kupata huduma bora za afya."
Alisema hospitali hiyo itakuwa na majengo 22. Hadi sasa majengo saba yamekamilika na mengine matatu yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Katika hatua nyingine, Chacha alisema serikali imetoa fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo la utawala la halmashauri hiyo.
Alisema, katika mwaka wa fedha 2020/2021 walipokea Sh milioni 750 na kwamba, wanajiandaa kupokea Sh bilioni moja ili kumaliza ujenzi.
"Karibuni tunakamilisha ujenzi jengo letu la utawala na eneo hili ambalo tunatumia kama ofisi zetu tutaligeuza na kuwa kituo cha afya… Serikali imeshatoa Sh milioni 250 na halmashauri kupitia mapato ya ndani tumetenga Sh milioni 258," alisema.
Alisema, kituo hicho cha afya kitahudumia wananchi wanaotoka katika Tarafa ya Mkuu ambao awali walikabiliana na ukosefu wa kituo cha afya hali iliyowalazimu kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hizo.