Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Serikali haijaagiza faini wanaojifungua nyumbani’

519cc062816726c5b9570cef9124415e ‘Serikali haijaagiza faini wanaojifungua nyumbani’

Fri, 12 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange amesema serikali haijatoa maelekezo yoyote kwa watendaji na watoa huduma za afya kutoza faini wakinamama wanaojifungua nyumbani.

Alisema hayo bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge Viti Maalumu (Chadema), Grace Tendega aliyetaka kujua kauli ya serikali kuhusu wajawazito wanaojifungua njiani au nyumbani kutozwa faini ya Sh 50,000 hadi 70,000.

Katika swali lake jingine, Mbunge huyo alisema imekuwa ni ahadi ya muda mrefu serikali kujenga sehemu za wajawazito kusubiria ambapo kwenye sera ya afya imesema itajenga vituo vya afya kila kata na zahanati kila kijiji.

Alisema katika Jimbo la Kalenga imekuwa kero kwa wakina mama wanaojifungua njiani au nyumbani kutozwa faini ya Sh 50,000 hadi 70,000 na kuhoji ni lini serikali itajenga majengo hayo na inasema nini kuhusu faini hizo.

Akijibu, Dk Ndugange alisema serikali haijatoa maelekezo kwa mtendaji au mtoa huduma yeyote wa afya kutoza faini hizo wakinamama wanapojifungua nyumbani.

Alisema ni wajibu wa watendaji katika mamlaka za serikali za mitaa kutoa elimu na kuhamasisha wajawazito kuona umuhimu wa kujifungua katika vituo vya kutolea huduma za afya badala ya kuwapiga faini ya kujifungua nje ya vituo vya huduma.

Aidha, aliwasisitiza wjawazito nchini kuendelea kujifungua kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Alisema vifo vya akinamama na watoto vinatakiwa kupunguzwa kwa kuboresha miundombinu ya afya yakiwamo majengo ya kusubiria.

"Ni kipaumbele cha serikali majengo hayo ya kusubiria yanajengwa ili kupunguza umbali wa wajawazito kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya," alisema.

Alisema ili majengo hayo yajengwe lazima kuwe na kituo cha afya na ndio sababu serikali inajenga kwa wingi vituo vya afya karibu na makazi ya wananchi na kwa maeneo yenye umbali mkubwa kuweka mpango wa pili wa kujenga majengo ya kujisubiria kujifungua.

"Haitakuwa na tija sana kujenga majengo ya kusubiria bila kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na umbali mkubwa kufuata huduma za afya, kipaumbele namba moja lazima kuwe na kituo cha afya, katika miaka hii mitano ndio maana serikali imejenga vituo vingi na tunaendelea na ujenzi huo ili kusogeza huduma kwa wananchi," alisema.

Dk Dugange alisema serikali imeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini, utekelezaji wa mpango huo umesaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya msingi na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa lengo la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga katika maeneo ya vijijini.

Alisema kuanzia 2015 hadi Septemba, 2020, serikali imejenga zahanati 1,198, imekarabati vituo vya afya 487 na kujenga Hospitali 102 za halmashauri.

Alisema ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya umesaidia kuongeza idadi ya wanaojifungua kwenye vituo vya afya kutoka milioni 1.38 mwaka 2015 hadi milioni 1.9 mwaka jana.

Alisema serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/21 imetenga Sh bilioni 27.75 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya zahanati 555 ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Chanzo: habarileo.co.tz