SERIKALI imeagiza wananchi wasikataliwe au kukosa chanjo ya corona kwa sababu zozote zile baada ya kufika katika kituo kwa nia ya kupata chanjo hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi alisema hayo jana katika taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari.
Profesa Makubi aliagiza watoa huduma katika vituo vyote vya kutolea chanjo hiyo watumie dakika chache kutoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo kwa wagonjwa wa magonjwa mengine.
Alisema hiyo itasaidia wananchi kuelewa na baadaye kufanya uamuzi sahihi kuhusu chanjo hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Makubi, hadi juzi Agosti 14 dozi 1,008,400 za chanjo hiyo zilikuwa zimesambazwa katika mikoa 26 katika vituo 550 vya kutolea chanjo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, hadi kufikia Jumamosi iliyopita, watu 207,391 wamepatiwa chanjo, kati yao, 121,002 ni wanaume sawa na asilimia 58.3 na 86,389 ni wanawake sawa na asilimia 41.7.
Aidha, pamoja na kupongeza kazi inayofanywa na mamlaka za mikoa, wilaya na mitaa ya kuhamasisha utoaji wa chanjo, alitoa rai kwa mamlaka hizo kuongeza juhudi za kutoa chanjo katika maeneo ya pembezoni ya miji, mitaa na vijiji.
Profesa Makubi aliwaasa wananchi waendelee kuchukua tahadhari za kinga kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka au kutumia vipukusi, wavae barakoa katika maeneo hatarishi na waepuke misongamano.
Utoaji wa chanjo ya corona kwa mikoa yote nchini ulianza Agosti 4, mwaka huu baada ya awali kutanguliwa na uzinduzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 28 mwaka huu Ikulu, Dar es Salaam.
Wakati huohuo, mkoa wa Dar es Salaam umepanga kuanzisha vituo vya dharura vya kutolea chanjo hiyo katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu.
Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Rashid Mfaume alisema kwa kuwa wananchi wengi wanatoka nyumbani usiku na kurudi usiku wanakosa nafasi ya kwenda katika vituo rasmi vya kutolea chanjo.
Alilieleza HabariLEO kuwa, ili kuwarahisishia wananchi hususani wanaokwenda katika maeneo yenye mikusanyiko kama vile Soko la Samaki la Feri na Soko Kuu la Kariakoo, serikali itaanzisha vituo vya dharura ili kuwapa chanjo watakaohitaji.
Aliwashukuru wananchi wanavyoendelea kujitokeza kupata chanjo na akahimiza wadau wakiwemo waandishi wa habari watumie kalamu zao kuhamasisha wananchi wakachanjwe.
Dk Mfaume alitaja mbinu nyingine ambazo serikali inazitumia ili kuongeza idadi ya watu watakaohitaji chanjo kuwa ni kutumia viongozi wa serikali za mitaa kutoa elimu ya umuhimu na ubora wa chanjo hiyo.
Alisema kwa kuwa serikali ya mtaa ni nyenzo ya kwanza katika kutatua matatizo ya wananchi, inaweza kutumika kuwashawishi kwa kuwa wapo nao mitaani.
Dk Mfaume alitaja mbinu nyingine kuwa ni kuwatumia madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda.