Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali: Hatutatumia nguvu, jilindeni na corona

Af5c9e7898dbfecc3c9d2cff2ea50448 Serikali: Hatutatumia nguvu, jilindeni na corona

Tue, 13 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amesema serikali haitatumia nguvu katika kukabilia wimbi la tatu la virusi vya corona, na badala yake watajikita katika utoaji elimu zaidi.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari jana Dar es Salaam lililoulizwa kuwa ni kwa nini mikusanyiko katika vyombo vya usafiri na matukio mbalimbali yanaendelea huku kukiwa na tishio la wimbi hilo, Dk Gwajima alisema bado wananchi wanatakiwa kuendelea kuelimishwa ili wajue jinsi ya kujikinga na kuepuka misongamano.

“Tumesema serikali haitatumia nguvu nyingi kuanza kukimbizana na watu tunachokilenga kwa sasa ni elimu kwanza itolewe iwafikie watabadilika,” alisema Dk Gwajima.

Aliongeza, “Tunahitaji vyombo vya habari visaidie kuelimisha na visaidiane na wakuu wa mikoa na wilaya kwani watu wengi wanakuwa hawajasikia kwa sababu tuna redio za kijamii sambazeni elimu watu wasikie watu wakishasikia watachukua tahadhari na wataacha wenyewe.”

Dk Gwajima alisema wapo watu walioelimika sasa wanavaa barakoa hivyo ni muhimu waandishi kufikisha elimu.

“Baada ya kutoa elimu hatua zitachukuliwa kwa watu ambazo wanapuuzia kwa sababu nao wanasababisha maambukizi yaendelee halafu tunachukua hela ambazo zingeweza kumtibu mtoto mchanga na mama mjamzito tunakwenda kununua mitungi ya oksijeni kuwaletea watu,” alisema Dk Gwajima.

“Lakini kwanza tuwaelimishe Watanzania serikali ina uwezo wa kuchukua hatua nyingi lakini hatua iliyoamua kuchukua kwanza na muhimu ni elimu,” aliongeza.

Julai 10, mwaka huu akiwa Dodoma, Dk Gwajima alibainisha kuwa hadi kufikia Julai 8, mwaka huu jumla ya wagonjwa 408 walikutwa na virusi vya corona huku wagonjwa 284 wakipumua kwa msaada wa mashine za oksijeni.

Chanzo: www.habarileo.co.tz