Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali: Hatujazuia utafiti magonjwa ya kupumua

Db7592712bfca0e6976050fd74eb0833 Serikali: Hatujazuia utafiti magonjwa ya kupumua

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema haijakataza utafiti katika eneo la tatizo la ugonjwa wa upumuaji (Covid 19) kama inavyosemekana mitaani ila watafiti wapo kazini.

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Abel Makubi alisema jana kuwa, kuna tafiti zilizofanyika na kuna mwongozo wa vipaumbele vya taifa.

Profesa Makubi alisema hayo alipofanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Upanga jijini Dar es Salaam.

Alisema kuhusu chanjo Rais John Magufuli alielekeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Maendeleo na Watoto kuwa makini kabla ya kuruhusu chanjo kwa kufanya utafiti wa kutosha ambapo ndilo jambo linalofanyika hivi sasa.

"Lazima tufanye utaratibu unaotakiwa. Taratibu zinaendelea kupitia wataalamu wetu hivi sasa tumeunda Kamati itakayotoa ushauri kwa serikali. Hatuwezi kwenda kiholela”alisema na kuongeza;

"Sio mara yetu ya kwanza kwenye suala la chanjo ila Watanzania tumekuwa wasahaulifu wa mambo. Alichokieleza Rais Magufuli kipo kinafanyiwa kazi kila kitu kina taratibu zake…wananchi msipotoshwe lakini pia muwe na subira watafiti wapo kazini".

Profesa Makubi alisema, serikali haiwezi kuacha wananchi wapate matatizo hivyo inataka kujiridhisha na chanjo badala ya kufuata mkumbo.

Alizitaka taasisi za MNH, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kuendelea kushirikiana kwa karibu katika eneo la chanjo.

Alisema nchi ina uwezo wa kutengeneza chanjo yake hivyo inapaswa kuwasaidia watafiti kwa sababu vifaa na wataalamu wapo.

Profesa Makubi akizungumzia suala la oksijeni alisema serikali inakabiliwa na uhaba katika hospitali zake nyingi nchini.

"Tuna uhitaji mkubwa wa oksjeni kama nchi, ni kama tulichelewa ilibidi kuwe na mitambo ya kusambaza oksijeni sababu tunauhitaji.

"Hivi tunashindwa kuchangishana mkasambaza kanda kanda ya pwani mpaka tusubiri serikali itupe hela za kufanyia hivyo?,"alihoji.

Alisema haoni sababu ya kila taasisi kujenga 'plant' yake peke yake ila MNH, MOI, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas) zinapaswa kuungana na kujenga moja kubwa ili wao wawe wasambazaji kwa wengine.

"Naamini mnaweza kukaa pamoja mkajenga plant kubwa ya oksijeni. Kuna vitu vingine ukiangalia havina shida ya soko,"alisema.

Awali Mkurugenzi Mkuu Profesa Lawrence Museru alisema wastani wa wagonjwa wa nje MNH ni 3500, kati ya hao wa Upanga ni 3000 na wa Mlonganzila ni 500.

Kuhusu wagonjwa wenye shida ya kupumua kwa tawi la Upanga alisema wamepungua na kufikia 37 hivi sasa na Mloganzila wanazidi kupungua.

Chanzo: www.habarileo.co.tz