Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekou Toure yazidiwa na wagonjwa

Mch Ed Sekou Toure yazidiwa na wagonjwa

Fri, 21 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mwanza Sekou toure imeelemewa na wagonjwa, baaada ya Serikali kuboresha miunombinu ya utoaji huduma ikiwamo upatikanaji wa vifaa tiba na dawa.

Hatua iliyosababisha wananchi wengi kwenda  huko kupata huduma badala ya kuanzia zahanati na vituo vya afya.

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Mkoa wa Mwanza,  Dk. Silas Wambura, alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kupokea msaada wa mashuka 200  yenye thamani ya Sh. milioni 2.5 yaliyotolewa na kampuni ya Insignia Ltd.

Alisema licha ya kuwapo mapungufu katika baadhi ya maeneo, lakini kwa sasa serikali imewekeza fedha nyingi katika miundombinu, vifaa tiba, dawa na watumishi ili kuhakikisha hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma bora.

Alisema kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya hospitali hiyo, wagonjwa wameongezeka, na kwamba wanafika mahali wanazidiwa na idadi hiyo.

Hata hivyo, alisema licha ya kuwa na wagonjwa wengi hakuna mtu anayefika huko na kukosa huduma anayohitaji  kwa kuwa hospitali hiyo imejipanga kulingana na rasilimali zilizopo.

Dk. Wambura alisema awali wananchi wengi walikuwa wanaanza matibabu katika hospitali za chini lakini kwa sasa wengi wanakwenda Sekou Toure bila kupitia huko.

Aliongeza kuwa hospitali hiyo inatarajia kujenga jengo la wagojwa wa nje, kukamilisha jengo la mama na mtoto pamoja na miundombinu mingine.

Aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza ili  kuisaidia hospitali hiyo katika maeneo mbalimbali,  ikiwamo miundombinu ya majengo, vifaa tiba,  vitanda, mashuka na  vitu vingine ambavyo vitasaidia kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Kampuni ya Insignia Ltd, Adam Kefa, alisema waliamua kutoa msaada wa mashuka baada ya kuombwa kufanya hivyo na Taasisi ya Doris Moleli.

Alisema licha ya mashuka hayo, pia kampuni yao iliamua kupaka rangi  jengo lote la watoto kwa gharama ya Sh. milioni 5.5.

Aliongeza kuwa msaada huo umetokana na faida wanayoipata na kuamua kuirudisha kwa jamii kwa kuboresha miundombinu katika hospitali hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live