Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sasa unaweza kupima Virusi vya Ukimwi ukiwa baa

50778 Pic+ukimwi

Sun, 7 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbali na huduma ya vinywaji, baa za maeneo mengi zinaweza kumpa mteja fursa ya kufanya manunuzi ya vitu tofauti; viatu, nguo, vifaa vya ufundi na vya ofisi na pia kuosha gari.

Lakini sasa usishangae kufuatwa na mtu ambaye atataka mazungumzo na mteja japo kwa dakika chache; ni mhudumu wa afya anayetaka kukushauri kuhusu afya yako, na hasa kupima Virusi vya Ukimwi (VVU).

“Mara ya kwanza niliwakuta wakiwa wanazungumza na washikaji (marafiki) zangu wakiwashauri kuwapima, niliona ni jambo la kushtua kidogo,” alisema Boniface Michael, mmoja wa wakazi wa Madale jijini Dar es Salaam.

“Watu wa aina hiyo kufika katika baa za pombe? Ilinichukua muda kuelewa na sikukubali.”

Alisema siku ya pili walifika kwa mara nyingine tena eneo hilo na kuendelea na kazi yao.

“Niliona huenda ni wakati muafaka kuwasikiliza zaidi na kuacha utani. Nikawaambia na wenzangu wafanye hivyo lakini ni kwa hiari wala si lazima,” alisema.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Calist Kessy alishangaa jinsi utaratibu huo ulivyoanza kimyakimya.

Alisema hatua hiyo ni nzuri, japokuwa jambo hilo linashtua kwa watu kwenda baa kufanya vipimo hasa wakati watu wameshakunywa.

Hata hivyo, hiyo ni sehemu ya mpango uliotangazwa na Serikali muda mrefu kuwa wataanza kuwafuata watu katika maeneo ya mikusanyiko ili kuwashauri kujua hali zao za afya kwa kupima Ukimwi, ingawa haikufirika kuwa mikusanyiko hiyo itahusu pia sehemu za starehe. “Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya tisini tatu,” alisema Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndungulile alipoulizwa na Mwananchi.

“Yaani asilimia 90 ya watu wote wanaoishi na VVU kutambua hali zao, asilimia 90 ya wenye maambukizi kuanza dawa na asilimia 90 ya walioanza dawa kupunguza kiwango cha VVU mwilini.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau tumeanza mkakati huu.”

Kampeni ya upimaji VVU na kuanza dawa inayowalenga wanaume ilizinduliwa Dodoma Juni 19 mwaka jana, wakati takwimu zikionyesha ni asilimia 45 pekee ya wanaume wanaoishi na VVU ndiyo wanaotambua kuwa wana maambukizi kwa mujibu wa utafiti wa NBS.

Dk Ndugulile alisema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua kampeni hiyo ya kitaifa ya “Furaha Yangu” yenye kaulimbiu ya “Mwanaume Jali Afya Yako, Pima VVU’ inayolenga kuwafikia wanaume ambao alisema wengi wao ni waoga kupima.

Alisema lengo la Serikali ni kujaribu kuangalia wapi wanaume walipo na kwamba si wizara pekee inayofanya huduma hiyo ila ni kwa kushirikiana na wadau.

Hata hivyo, Dk Ndugulile alisema upimaji huo haufanyiki kwa kwenda nyumba kwa nyumba.



Chanzo: mwananchi.co.tz