Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saratani ya macho kwa watoto yatajwa kuwa tishio Tanzania

Sun, 19 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya kuwa saratani ya macho kwa watoto ni ugonjwa usiofahamika zaidi kwenye jamii, unatajwa kuwa miongoni mwa magonjwa tishio nchini Tanzania.

Wastani wa watoto 60 hadi 80 kwa mwaka hufikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya tatizo hilo linalosababisha upofu na vifo.

Hayo yameelezwa leo Mei 17, 2019 na daktari bingwa wa macho,  Dk Anna Sanyiwa wakati wa uchunguzi wa saratani ya macho kwa watoto katika hospitali ya Mloganzila ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya kimataifa ya saratani ya macho kwa watoto.

Amesema tatizo hilo ni kubwa tofauti na wengi wanavyodhani ila changamoto ni kwamba watoto hufikishwa hospitali wakiwa kwenye hatua mbaya.

Amesema katika hospitali ya MNH aina hiyo ya saratani ni ya pili kwa kuwa na wagonjwa wengi waliopo wodini.

“Huu ugonjwa upo na unatibika ukiwahi mapema hospitali, tatizo ni kwamba wanaletwa wakiwa tayari wameathirika vibaya na ikifika hatua hiyo ni ngumu kutibu,”

Pia Soma

Dk Sanyiwa amesema ni muhimu kwa wazazi kuwachunguza watoto wao na kuwafikisha mapema hospitali wanapoona tofauti.

“Ukiona mtoto ana kengeza au weupe kwenye jicho usione ni kitu cha kawaida mpeleke hospitali afanyiwe uchunguzi,  ukimchelewesha jicho linaharibika na inaweza kusababisha hadi kifo,” amesema Dk Sanyiwa

Chanzo: mwananchi.co.tz