Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sampuli za chakula walichokula watoto na kufa zapelekwa kwa Mkemia

D067c2ee957846a8542e8ee575db9174 Sampuli za chakula walichokula watoto na kufa zapelekwa kwa Mkemia

Sun, 23 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Katavi, Dk Yusta Tzeba amesema sampuli za watoto watatu wa familia moja waliokufa baada ya kula kunde pori na viazi vitamu walizozichuma porini na kupika wao wenyewe zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini kitabibu aina ya sumu iliyosababisha vifo vyao.

Watoto hao wa familia moja walifikwa na umauti baada ya kula viazi vitamu na maharage pori vinavyosadikiwa kuwa na sumu na kutambuliwa kuwa ni Kabula Yohana (6),Modesta Makoye (4) na Ezekiel Yohana (3) ambao walikuwa wakiishi katika kijiji cha Igongwe wilayani Mpanda.

Wengine watatu wa familia hiyo pia wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Katavi kwa matibabu na hali zao zikielezwa kuwa zinaendelea kuimarika Akizungumza na gazeti katika mahojiano maalumu yaliyofanyika kwa njia ya simu Dk Tzeba alisema kuwa sampuli za watoto hao zilitumwa Alhamisi asubuhi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali .

“Majibu yatatolewa baada ya miezi miwili au mitatu inategemeana na aina ya sampuli zenyewe na umbali uliopo kutoka huku... tumezipeleka sampuli hizo tangu Alhamisi asubuhi,” alifafanua na kuongeza kuwa baada ya miili ya watoto hao kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ilikabidhiwa kwa ndugu zao kwa maandalizi ya maziko.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Benjamin Kuzaga akizungumza na wanahabari Agosti 18,mwaka huualisema mkasa huo ulitokea Agosti 16,mwaka huu saa kumi na mbili jioni katika kijiji cha Igongwe, kata ya Stalike, tarafa ya Nsimbo, wilaya Mpanda mkoa wa Katavi.

Akisimulia mkasa huo alisema siku hiyo ya tukio watoto hao wakiwa pamoja na watoto wengine watatu ambao ni Yona Sabuni (4),Christina Yohana (4) na Paulo Yohana (6) kwa pamoja walienda kuchuma mbegu za mmea pori mfano wa kunde na kula pamoja na viazi vitamu walivyopika wao wenyewe na baada ya muda hali zao zilibadilika na kuanza kuhisi maumivu makali ya tumbo wakati huo wazazi wa watoto hao ambao ni Yohana Ellias na Agnes Lucas walikuwa shambani na hivyo kukosa msaada wa haraka.

Aliongeza kuwa, “ ilipofika 12:30 walikutwa na jirani aitwaye Amos Antony wakiwa wamelala chini huku wakilalamika wakihisi maumivu makali ya tumbo.”

Chanzo: habarileo.co.tz