Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sampuli 100 dawa za asili zafanyiwa uchunguzi

Dawa Asilia Sampuli Sampuli 100 dawa za asili zafanyiwa uchunguzi

Wed, 31 Aug 2022 Chanzo: mwananchi

Takribani sampuli 100 za dawa asili zilizowasilishwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 na wataalaamu wa tiba asili na tiba mbadala zilifanyiwa uchunguzi na kati ya hizo asilimia 80 ya zilikidhi ubora wa kimataifa.

Meneja Maabara Chakula na Dawa Ofisi ya Mkemia mkuu wa serikali (GCLA), Dk Shimo Peter ameyasema hayo jana Agosti 30, 2022 mjini Morogoro katika maadhimisho ya wiki ya tiba asili ya Mwafrika ukanda wa Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Dk Shimo amesema asilimia 20 ya sampuli hazikukidhi viwango vya ubora wa kimataifa na wataalamu wa dawa asili hizo walishauriwa kuboresha mifumo yao ya uzalishaji ili wazalishe dawa ambazo ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita dawa za asili zimekuwa zikiongezeka kutokana na wataalamu wa dawa asili kuwasilisha dawa zao Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili zifanyiwe uchunguzi wa kimaabara.

Dk Shimo alitolea mfano katika wimbi ya Covid -19, takwimu zinaonesha dawa asili nyingi kutoka kwa wataalamu wa dawa asili ziliwasilishwa kwa mkemia mkuu wa serikali ili kufanyiwa uchunguzi na baadhi zilifanikiwa kukidhi ubora na nyingine hazikukidhi.

Pia amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya matumizi holela ya dawa za asili jambo linaloweza kusababaisha vifo na madhara mengine kwa watumiaji na kutahadharisha wananchi kuacha kutumia dawa kiholela.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi za Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira kutoka Ofisi hiyo, Sabanitho Mtega aliwataka waganga wa tiba asili na tiba mbadala wanaotoa huduma hizo kusajili dawa zao baada ya kuthibitishiwa ubora wake ili kudhibiti matukio na athari za sumu zinazotokana na dawa hizo .

Licha ya kauli hiyo alisema katika kipindi cha sasa wengi wa waganga wa tiba asili na tiba mbadala wanajitokeza kupata huduma ya kufanyiwa upimaji wa dawa asili ili kubaini usalama au laa kwa matumizi ya binadamu.

“Bila kufanyiwa uchunguzi wa dawa zao na kuidhinishiwa ubora wake ina wawia vigumu wao kupata usajili wa huduma ya tiba asili na tiba mbadala, kuwezesha dawa zao kusajiliwa na kupata kibali ili wauze kihalali,” amesema Mtega

Kurugenzi hiyo ina maabara nne ambazo ni maabara ya chakula, dawa, maikrobaiolojia na mazingira zikiwa na majukumu tofauti ikiwemo kufanya uchunguzi wa kikemia na kimaikrobaiolojia kwa sampuli za vyakula, vinywaji na mazao ya kilimo, mifugo na malighafi zake, sampuli za dawa za kisasa (Pharmaceuticals), dawa asili na malighafi zake.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Miongo Miwili ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika"Kuelekea Huduma ya Afya kwa Wote ambayo yamendaliwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Umoja wa Watengenezaji Bidhaa za Asili Tanzania (Uwabiata).

Chanzo: mwananchi