Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia asema maambukizi ya TB yamepungua Tanzania

83368 SAM Samia asema maambukizi ya TB yamepungua Tanzania

Mon, 11 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makamu wa Rais nchini Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema maambukizi mapya ya Kifua Kikuu (TB) nchini yamepungua kwa asilimia 4.6 kwa mwaka.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 7, 2019 wakati akifungua mkutano wa mawaziri wa sekta ya afya na Ukimwi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

“Vifo vitokanavyo na TB vimepungua kutoka 55,000 mwaka 2015 hadi 39,000 mwaka 2018 ambavyo ni sawa na asilimia 27, lakini utoaji wa taarifa za wenye ugonjwa huu umeongezeka kwa asimilia 20.6 kutoka mwaka 2015 hadi 2018,” amesema Samia.

Amesema hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa kiwango cha utambuzi wa ugonjwa wa TB kutoka asilimia 37 mwaka 2015 na kufikia asilimia 53 mwaka 2018.

Samia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi yenye kiwango cha chini cha usugu wa dawa za TB kwa kuwa na asilimia 0.3 ya usugu kwa wenye maambukizi mapya na asilimia 13 kwa wagonjwa waliotibiwa.

“Hadi Septemba 2019 vituo 103 vinatoa huduma ya tiba kwa wagonjwa wenye TB sugu ikilinganisha na kituo kimoja mwaka 2015.” “Mashine 232 zenye teknolojia mpya ya  GeneXpert ambayo inatoa majibu ndani ya saa mbili zimefungwa kwenye vituo vya afya katika mikoa yote nchini,” amesema Samia.

Amebainisha kuwa pamoja na kuongezeka kwa utoaji wa taarifa za wenye TB, bado kuna changamoto kati ya idadi ya wagonjwa waliotolewa taarifa na makisio ya idadi ya wagonjwa wenye maambukizi mapya.

Chanzo: mwananchi.co.tz