Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia Suluhu atoa tahadhari ugonjwa wa ebola Kigoma

16658 Pic+samia TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uvinza. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi mkoani Kigoma kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ebola kwa kutokumbatia wageni wanaotoka nchi ya jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). 

Aidha, amewataka wafanyabiashara ya dagaa mkoani humo kujiunga katika vikundi ili kuwa na kauli moja katika bei ya bidhaa hiyo.

Makamu wa Rais aliyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi katika Bwalo la Muyobozi eneo la kuvulia dagaa na samaki, kata ya Mwakizega wilayani hapa, akiwa katika ziara ya siku nne mkoani Kigoma iliyoanza jana.

amesema ni vizuri wananchi wakachukua hatua ya kuzuia ugonjwa huo kwa hatua za awali. 

Alisema mkoa wa Kigoma upo karibu na DRC na kwamba inachukua takribani saa tatu kufika nchini humo hivyo ni muhimu wananchi kuacha kupokea wageni kiholela na kuwahifadhi. 

"Niwaombe mchukue tahadhari mapema juu ya ugonjwa huo, kwa kuwa makini na watu mnaowapokea na kukutana nao, kwani pia kuna mwingiliano mkubwa wa watu baina ya nchi hizi mbili, tahadhari ni muhimu," alisema.

Kwa upande wa wafanyabiashara ya dagaa, alisema ni vizuri wakafanya utaratibu wa kukaa katika vikundi kwani hata wakulima wa zao la korosho walikuwa wakilalamika kulanguliwa katika zao hilo lakini baada ya kufanya hivyo wamekuwa na bei moja elekezi. 

"Niwaombe mkae katika vikundi ambavyo kupitia hivyo mtaweza kuwa na kauli moja ambayo itawapelekea kuwa na bei elekezi na kuepukana na walanguzi," alisema

Akijibu ombi la Mkurugenzi wa halmshauri hiyo, Weje Ng'oro la kumtaka kufanya eneo hilo kuwa kituo cha forodha, Samia alisema ombi hilo amelichukua na atalifanyia kazi lakini sio kwa sasa. 

Alisema kituo cha forodha kinatakiwa kiwe bize muda wote watu wakiwa wanafanyakazi lakini baada ya kuona hakuna shughuli zinazoendelea hapo hataweza kukifanya kituo kwasasa mpaka atakapotuma watu kukikagua na kujiridhisha. 

 

 

"Kwasasa sitaweza kuruhusu kuwa kituo cha forodha mpaka nijiridhishe maana toka nimefika hapa naona eneo haliko bize hakuna watu wanaofanya shughuli zozote, ila ombi lenu nalichukua na nitatuma watu waje wakague," alisema Samia.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmuel Maganga, aliwataka wananchi wa mkoa huo wasiwalee wala kuwakumbatia wageni ambao hawawajui katika maeneo yao na badala yake watoe taarifa haraka katika mamlaka husika. 

"Msishikane mikono na mtu yeyote lengo ni kujikinga na ugonjwa wa ebola kwani asili ya mkoa wetu uko mpakani kabisa na nchi jirani ya Kidemokrasia ya Congo na ni rahisi kupata ugonjwa huo, tahadhari ni muhimu sana,” alisema  

Mkuu wa wilaya hiyo, Mwanamvua Mlindoko alisema katika wilaya hiyo wanapokea wahamiaji wasio rasmi 190 kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Chanzo: mwananchi.co.tz