Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Samaki wanaokufa Ziwa Victoria hawana sumu’

829901fb39fe973509ec6c93e4af2f9b ‘Samaki wanaokufa Ziwa Victoria hawana sumu’

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

S ERIKALI imesema samaki wanaokufa katika Ziwa Victoria hawana sumu, lakini haishauri watu wawatumie kwa kitoweo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Rashid Tamatama, aliyasema hayo juzi na kueleza kuwa, baada ya uchunguzi wa sampuli walizopeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, majibu yameonesha samaki hao hawana sumu.

Mwezi mmoja uliopita, samaki aina ya sangara wanaoweza kukua na kufikia zaidi ya kilogramu 100 walionekana wakielea majini wakiwa wamekufa katika ziwa hilo maeneo ya Kenya na Uganda. Dk Tamatama alisema wiki moja baada ya samaki hao kuonekana wamekufa, walifanya uchunguzi kuanzia Rorya hadi Bukoba.

“Kwa takribani wiki mbili sasa, maeneo ya Rorya na Bukoba samaki wengi wameonekana wakiwa wamekufa sababu ilikuwa haijulikani, hali hiyo ilianza kutokea mwezi mmoja uliopita katika maeneo ya Kenya na Uganda,” alisema.

Alisema walichukua sampuli katika maeneo ya Musoma, Nyamikoma, Sengerema, Geita, Bukoba na kuzipeleka kwa mkemia mkuu ili kuangalia kama zina sumu au walikufa kifo cha kawaida.

“Matokeo yanaonesha hakuna samaki yoyote aliyekutwa na sumu, inathibitisha alichoongea Dk Ishmael Kimerei kuwa wamekufa kwa kukosa hewa kwa sababu kwenye Ziwa Victoria yale maji huwa muda wote kuna leya ya maji ya chini hayachanganyiki na leya ya maji ya juu,” alisema.

Dk Tamatama alisema katika ziwa hilo maji ya chini joto lake lipo chini na ya juu mara nyingi joto ni la juu. “Ziwa Victoria kuanzia mita 20 oksijeni huwa haipo, kwa muda mrefu hayo maji yanakaa hivyo leya mbili hazichanganyiki, sasa kuna muda hali ya tabianchi ziwani maji yanachanganyika ya juu yanaenda chini na ya chini yanaenda juu hasa miezi ya baridi na kipupwe,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk Tamatama, maji ya chini ni mengi kuliko ya juu na yakipanda juu yanakuwa hayana oksijeni hivyo kuwaathiri samaki na kwamba, wanaoathirika zaidi ni samaki wakubwa kama sangara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz