Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata zahanati kuwabebesha uchafu wazazi latua Wizara ya Afya

Wed, 17 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Same. Sakata la Zahanati ya Bwambo iliyopo kijiji cha Bwambo wilayani Same, Kilimanjaro la kuwataka wazazi kuondoka na uchafu baada ya kujifungua, limechukua sura mpya baada ya Serikali kutoa agizo zito kwa uongozi.

Wiki iliyopita, muuguzi wa zahanati hiyo, Merrystella Msuya aliliambia Mwananchi kuwa tatizo hilo ni la muda mrefu na kwamba wamekuwa wakijisikia vibaya kuwataka wazazi kuondoka na uchafu baada ya kujifungua. “Zahanati hii haina choo wala maji, kwa hiyo akinamama wakijifungua hapa inatulazimu tuwaambie wabebe taka zao wapeleke nyumbani, nadhani hii sio sahihi,” alisema Merrystella.

Akizungumza na Mwananchi jana, naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema kwa mujibu na taratibu za vituo vyote vinavyotoa huduma za afya, ni lazima viwe na sehemu ya kuchomea taka hizo, vyoo na maji ya uhakika.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa baada ya zahanati hiyo kutokuwa na vifaa vya kuhifadhia taka ngumu na huduma ya maji safi na salama.

Naibu waziri huyo alisema kitendo cha kuwabebesha wazazi uchafu baada ya kujifungua ni kinyume cha utaratibu.

Alisema ili zahanati isajiliwe ni lazima ikidhi vigezo vyote vilivyowekwa na wizara vikiwamo vya kuwa na huduma alizozitaja hapo juu.

“Kimsingi jambo hili lililofanyika ni kinyume cha taratibu kwa sababu ili zahanati ikamilike ni lazima iwe imekidhi vigezo vyote, hili jambo tutalichukulia hatua haraka kwa sababu linahatarisha afya ya mama na mtoto, na naliomba jambo hili nipeleke sehemu husika,” alisema Dk Ndugulile.

Mganga mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Besti Magoma alisema suala hilo amelipata na ofisi yake imeshawasiliana na mganga mkuu wa wilaya pamoja na kutoa maelekezo ya kulishughulikia haraka iwezekanavyo.

“Tayari ofisi yangu imekwishawasiliana na mganga mkuu wa wilaya hiyo na kutoa maelekezo ya kushughulikia suala hilo haraka, pamoja na kupata taarifa za kina nini kilisababisha kuwe na hali hiyo,” alisema Dk Magoma.

DC na DED wanasemaje

Alipoulizwa juu ya suala hilo, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Same, Anna Shija alisema hana taarifa juu ya tatizo hilo na kuahidi kufuatilia.

Lakini mkuu wa wilaya hiyo, Rosemary Senyamule alishangaa zahanati kukosa huduma muhimu kama hiyo akisema hana uhakika kama zahanati hiyo inafanya mchezo huo wa aibu wa kuwabebesha wazazi uchafu.

“Nashangaa zahanati haina shimo la kuchomea taka, maji pamoja na choo. Nitafuatilia taarifa hizo ili niweze kuzifahamu zaidi,” alisema Senyamule.

NGO zawalilia wazazi

Mratibu wa taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania, Rose Mlay alisema kitendo cha kumbebesha uchafu mzazi ikiwemo kondo la nyuma baada ya kujifungua ili akatupe nyumbani kwake si sahihi na ni tishio kwa afya yake na wengine.

Alisema mtu anayekwenda kutupa uchafu huo kama si mgonjwa anaweza kuambukizwa maradhi mbalimbali kutokana na kutokuwapo iwapo mzazi alikuwa na maradhi. “Si vizuri kumbebesha mama kondo la nyuma kwa sababu hujui nani anakwenda kulishika, sasa hivi kuna magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi, mtu akishika ile damu ni rahisi kupata maambukizi,” alisema Mlay.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na na utetezi wa haki za binadamu katika jamii (Ajiso), Virginia Silayo aliitaka halmashauri hiyo kujenga vyoo na shimo la kutupia taka hatarishi katika zahanati hiyo. Wiki iliyopita, Mwananchi lilifika katika zahanati hiyo na kushuhudia chumba cha kujifungulia hakina maji wala choo. Pia hakukuwa na shimo katika eneo la zahanati kwa ajili ya kuchomea taka hatarishi kama ilivyo katika maeneo mengine.

Chanzo: mwananchi.co.tz