Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Safari yangu ya miaka 22 na kisukari—Dk Sebalua

9555 Safari+pic.png TZWeb

Wed, 20 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ilikuwa saa moja asubuhi, mzee mmoja anaketi kwenye benchi la chuma katika hali ya uchovu huku macho yake yakiwa yamefunga.

Ameketi nyuma ya mlango wa kuingia chumba cha kusafishia damu. Pembeni kukiwa na wagonjwa wengine saba, mzee huyu anasaidiwa kujiandaa kwa ajili ya matibabu anayoendelea nayo maishani mwake. “Siyo mbaya kama vile inavyoonekana,” anasema Martin Sebalua mwenye miaka 67 ambaye ni daktari mstaafu na kuongeza: “Lakini ni ugonjwa ambao nisingependa hata kidogo mtu yeyote aupitie.”

Baada ya kuingia kwenye chumba cha matibabu, Dk Sebalua akiwa amejinyosha kwenye kitanda, anaonekana kuwa katika hali ya utulivu, licha ya kwamba mwili wake ulikuwa umezungukwa na mirija iliyounganishwa na mashine ya kusafishia figo ambayo ni vigumu kuitambua.

Huku akinyanyua shuka yake nyeupe, mirija myembamba inaunganishwa kwenye mashine ya kusafishia damu iliyoko upande wa kushoto ikitoa na kuingiza damu mwilini mwake. Inaonyesha ni hali yenye maumivu na taabu kwa jinsi alivyokuwa akionekana.

Daktari huyu anasumbuliwa na kisukari kwa miaka 22 sasa na aligundulika akiwa katika hatua za mwisho na tayari figo yake ilikuwa imeshaathirika tangu mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Sebalua ni miongoni mwa watu milioni 422 duniani wenye matatizo ya kisukari, huku wengine milioni 1.6 wakifariki dunia kila mwaka kutokana na maradhi hayo.

“Hakuna mtu anayependa kutumia muda wake hospitalini na hasa inapokuwa mara tatu kwa wiki,” anasema na kuongeza, lakini unapaswa kuja kupata matibabu ya namna hii kwa sababu ndiyo tegemeo la maisha yako.”

Kwa kipindi cha miaka mitatu sasa, Dk Sebalua amekuwa akihudhuria kliniki hii kwa ajili ya kusafisha damu yake na amekuwa akifanya hivyo kila siku za Jumanne, Alhamisi na Jumamosi na hutumia muda wa saa nne akiwa kitandani ili kazi hiyo ikamilike. “Usafishaji wa damu umeniwezesha kufika hapa nilipo, lakini moyoni natambua mwili wangu umeshindwa kabisa kwa sababu hakuna tiba ya ugonjwa huu (kisukari) - siyo jambo rahisi kuishi kwa kutegemea msaada wa mashine,” anaeleza akiwa katika hali ya kutia huruma.

Dk Sebalua anasema usafishaji wa damu ni mchakato unaohusisha ukaushaji.

“Unaona mashine hii inafanya kazi kama mbadala wa figo. Nimefikia hatua ambayo sina uwezo wa kutoa mkojo na vitu vingine vinavyozalishwa mwilini, hivyo mashine huondoa damu kutoka mwilini ambako sumu huondolewa na kisha huirejesha damu hiyo ikiwa imechujwa na safi mwilini.

Inafanya kazi hatua kwa hatua. Na mgonjwa anapewa matibabu yake katika vipindi vitatu kwa wiki. “Nachoka kila baada ya kipindi kimoja, hakuna namna lazima nifanye ndiyo tiba,” anasema.

Kisukari kilivyombadili daktari kuwa mgonjwa

Dk Sebalua alikuwa kila kitu, hasa unapofikiria daktari anapokuwa katika umri wa miaka ya 40. Alikuwa kwenye kiwango cha juu akifanya kazi kwa weledi na kujituma akiwa daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

Lakini miaka 22 iliyopita, maisha yalibadilika kabisa wakati alipogundulika kuwa na tatizo la kisukari. Alikuwa tayari amepitia karibu dalili zote za mtu anayetaka kuugua ugonjwa sukari.

Anasema alianza kupata mkojo wa mara kwa mara, maumivu ya misuli na kiu ya kila wakati. Zilikuwa dalili za tatizo hilo. “Hizo zilikuwa hisia zangu za kwanza kuwa kwa vyovyote vile, hali hii imetokana na mfumo wangu wa maisha,” anasema.

Ingawa hawezi kukumbuka bayana kisa kimojawapo, lakini anakiri mfumo wa maisha yake kwa ujumla haukuwa mzuri kiafya. “Nilikuwa mnywaji mkubwa wa pombe, nilipenda sana kunywa bia na wala sikuzingatia kabisa suala la kula vizuri, sikuwa na mazoezi, nilikuwa na mambo mengi kazini kiasi cha kunisababishia kuwa na msongo wa mawazo, pia nilikuwa mnene katika umri ule,” anasema.

Hata hivyo, hueda ikawa siyo sababu moja tu, bali kukawa na sababu nyingine nyingi zilizomfanya Dk Sebalua kukumbwa na tatizo la kisukari na baadaye kutumbukia kwenye matatizo mengine. Anasema wakati alipoaanza kuugua, alikuwa tayari ameoa na kujaliwa watoto wanne. Familia pamoja na marafiki zake walimshauri kuanza kuchukua tahadhari kuhusu mwenendo wake wa ulaji. “Unapotakiwa kubadili ghafla mfumo wako wa maisha na jinsi ya ulaji wakati tayari umeshafikisha miaka 40, ni changamoto kweli, na inavunja moyo. Yaani unahisi kama vile umetengwa na watu wako wa karibu....unapikiwa chakula cha peke yako na maisha mengine kabisa. Nililazimika kuachakula vyakula vyenye wanga, matumizi ya sukari, vyakula vya mafuta na kuanza kutumia vyakula vya kawaida kabisa,” anasimulia.

Mwaka 2013 maisha yake yalibadilika

Miaka 17 baada ya kugundulika kuwa ana kisukari hatua ya pili, figo ya Dk Sebalua ilikuwa imepoteza nguvu ya kufanya kazi, tatizo ambalo linawaandama watu wengi wenye matatizo ya kisukari nchini.

“Niliona mwili wangu ukiumuka nikajua kuna kitu hapa hakipo sawa. Nilikuwa katika majonzi makubwa.

Miaka yote hii nilikuwa mwangalifu juu ya afya yangu nikiwa na matumaini ya kupungua uzito, lakini haikusaidia kitu.”

Kisukari ni ugonjwa ambao ukicheleweshwa kutibiwa, huleta madhara makubwa kwa mgonjwa. Na mgonjwa hawezi kuwa na uhakika wa moja kwa moja wa kupona. Wakati Dk Sebalua alipofika Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake, mtaalamu wa figo alimwambia tatizo lake limefikia hatua ya Tano ambayo ni ya mwisho. Mwaka huo aliamua kustaafu kazi. “Niliambiwa nimtafute mtu wa kujitolea figo yake ili nipandikizwe, ikiwa ndilo suluhisho lililodhaniwa. “Bahati nzuri wakati ule Wizara ya Afya ilikuwa na uhusiano na hospitali kadhaa za India ambazo zingeweza kufadhili wagonjwa kama mie wa upandikizaji wa figo, lakini huduma hiyo ilikuwa haitolewi tena,” anasema akiongeza kilio cha wagonjwa wengi nchini wenye tatizo kama lake lililofikia hatua ya mwisho na wanashindwa kupata matibabu kutokana na gharama kubwa. Sababu mojawapo ya wagonjwa wengi wa figo hasa wale wenye kipato cha chini kutojua kuhusu upandikizaji wa figo ni kutokana na madaktari wao kushindwa kuwaeleza bayana kwamba suala la upandikizaji wa figo linawezekana na ni uamuzi wa mtu. “Mtoto wangu wa pili anayeitwa Martha aliamua kujitolea figo yake moja ili nipandikizwe mimi na alisema yuko tayari kuishi na figo moja ili mimi niondokane na tatizo hili.”

Kwa nini Dk Sebalua bado anaendelea na usafishaji wa damu wakati alishapewa rufaa ya kwenda India kwa ufadhili wa serikali kwa ajili ya kupandikizwa figo mpya?

“Dar es Salaam madaktari hawakugundua jambo moja muhimu ambalo liligundulika India baada ya kufanyiwa vipimo,” anasema Dk Sebalua na kuongeza; “Kulikuwa na tatizo la kuziba kwenye moyo wangu lililosababishwa na kisukari.”

Dk Sebalua alitumia muda wa miezi saba nchini India akitumia Sh47 milioni kwa ajili ya matibabu yaliyohusisha operesheni ya moyo na kuzibua mirija iliyoziba jambo ambalo lilimfanya ashindwe kupata huduma ya kupandikiziwa figo. Aliambiwa arejea nyumbani Tanzania aendelea kupata matibabu na kupumzika. “Muda ushakwenda kwa mimi kufanyiwa upandikizaji wa figo, nimeshakuwa mzee na nisingependa kuyaweka hatarini maisha ya binti yangu,” anasema Dk Sebalua akiwa tayari amekata tamaa.

Makala haya iliandikwa kwa lugha ya Kiingereza na kutafsiriwa na George Njogopa

Chanzo: mwananchi.co.tz