Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Safari ya kilomita zaidi ya 40 kusaka huduma za afya

Wasafirri Kilimoeta.png Safari ya kilomita zaidi ya 40 kusaka huduma za afya

Wed, 11 Oct 2023 Chanzo: mwanachidigital

Je, lini Serikali itajenga vituo vya afya katika kata za Mlembule, Godegode, Chunyu na Berege?

Ni swali namba 113 la George Malima, Mbunge wa Mpwapwa alilouliza kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), katika mkutano wa 12 wa Bunge, kikao cha nane Septemba 7, mwaka huu.

Naibu waziri wa wizara hiyo, Dk Festo Dugange alijibu ifuatavyo:

“Serikali inatambua mahitaji ya vituo vya afya katika kata za kimkakati kote nchini. Katika kipindi cha miaka mitano imetekeleza ujenzi wa vituo 2,406 vya kutolea huduma za afya ambavyo bado vina uhitaji wa baadhi ya miundombinu, ikiwemo vifaatiba na watumishi.

“Serikali itaendelea kutenga kwa awamu fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati kote nchini, zikiwemo kata za Godegode, Chunyu na Berege katika Halmashauri ya Mpwapwa.”

Majibu haya ya wizara yananikumbusha jambo, naiwaza Kata ya Godegode iliyopo Mpwapwa ikiwa mpakani mwa mikoa ya Morogoro na Dodoma upande wa Kusini Mashariki, pia ipo mwisho kwa jimbo la Mpwapwa kuelekea Kibakwe.

Godegode ina wakazi 11,150 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Ina vijiji vinne na vitongoji 14.

Katika tafakuri ya kina, nakumbuka namna wananchi wanavyokabiliwa na changamoto wakati wa mvua, hata Shirika la Reli Tanzania (TRC) mara kadhaa hulazimika kusitisha safari kutokana na kuharibika miundombinu yake katika eneo hili.

Kata hii inazungukwa na Mto Kinyasungwi, ambao unapofurika katika msimu wa mvua hubomoa reli kipande cha Godegode – Kidete au Godegode – Gulwe.

Ni kutokana na hali hiyo, daraja la Godegode kwa miaka mingi sasa limevunjika, hivyo hakuna usafiri wa moja kwa moja kwenda Mpwapwa.

Wananchi wanatumia barabara ya muda iliyochongwa katika mradi wa reli ya kisasa kupitia Gulwe na kuunganisha barabara ya Kibakwe ambayo msimu wa mvua haipitiki.

Kata hii haina kituo cha afya; huku vijiji vya Kisisi na Mzogole vikiwa havina zahanati, Godegode pekee ndiko kuna zahanati.

Kijiji cha Mgoma kuna zahanati iliyojengwa kwa nguvu ya wananchi na msaada wa Serikali, lakini utendaji kazi wake bado ni wa kusuasua kwa kuwa baadhi ya miundombinu haijakamili.

Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Juni 2007, zahanati inapaswa kuwapo kwenye kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata, hospitali kwa kila wilaya, hospitali ya rufaa kila mkoa na hospitali maalumu ngazi ya Taifa.

Kwa ujumla, vituo vya afya na zahanati ndiyo ngazi ya kwanza za afya inayoigusa jamii moja kwa moja.

Kutokana na changamoto zilizopo katika kata hii, wajawazito huathirika zaidi wakilazimika kuhamishia makazi Mpwapwa kusubiri kujifungua; huku baadhi ya wanajamii wamegeukia tiba mbadala kukwepa gharama za kufuata tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.

Kwa wajawazito wasiohamisha makazi, hutumia takribani Sh40,000 kwa ajili ya kukodi pikipiki kusafiri umbali wa kilomita zaidi ya 40 kufuata huduma kwenye hospitali ya wilaya.

Wasemavyo wananchi

Velyani Khalifa (28), aliyepoteza mtoto mchanga wa siku moja, anaeleza kuwa hilo lilitokea kwa kuwa alichelewa kufika hospitalini kujifungua.

Anasema ilikuwa ni uzazi wake wa kwanza, hivyo hakujua, hata aliposhauriwa akapange chumba mjini Mpwapwa ili awe jirani na hospitali alipuuza.

“Nilikwenda hospitali kwa kutumia pikipiki baada ya kushikwa na uchungu, tulifika mtoto akiwa amechoka, nilifanyiwa upasuaji, mtoto alianza kupumua kwa mashine, baadaye akapoteza maisha,” anasimulia Velyani.

Anasema madaktari walimpa sababu mbili zilizosababisha mtoto wake azaliwe dhaifu; mosi, kuchelewa kituo cha huduma na pili, mwendo mrefu wa kukaa kwenye pikipiki akiwa na uchungu wa kuzaa.

Iwapo kungekuwa na huduma jirani, anasema madhila hayo yasingemfika kwa kuwa alishaelezwa kliniki kuwa hakuwa na tatizo katika ujauzito.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisisi, Samuel Chihongwe anasema hakuna gari linaloweza kufika kijijini hapo na kwamba, kipindi cha masika hata usafiri wa pikipiki ni tatizo.

Kwa mujibu wa Chihongwe, walitenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati lakini utekelezaji umekuwa mgumu.

Kwa upande wa wajawazito, anasema wanapofikisha miezi minane huweka kambi Mpwapwa mjini ili kuwa jirani na huduma za hospitali, lakini wengine hutenga kati ya Sh25,000 na Sh40,000 kwa ajili ya usafiri wa pikipiki muda wa kujifungua unapowadia.

“Hapa huwezi kupitisha hata gari la wagonjwa, vinginevyo abebwe umbali wa kilomita nane kutafuta barabara ndipo safari ianze, kwa ujumla tupo katika dunia nyingine tofauti na wenzetu,” ananieleza.

Anasema kwenye eneo hilo hukabiliwa na changamoto za wanafunzi kuugua ghafla, hivyo huchangishana fedha na kuwapeleka Mpwapwa au Kituo cha Afya Pwaga, umbali wa takribani kilomita 12.

“Ukisema nikakae Mpwapwa siwezi kwa kuwa kuna gharama kubwa, nahitaji mtu wa kunisaidia,” anaeleza Flora Meshack.

Anasema watoto wawili aliwazaa bila shida; mmoja kwa mkunga kijijini na wa pili alitumia pikipiki kwenda hospitali ya Mpwapwa.

Kilichomponza asipate mtoto wa tatu, anasema ni kusubiri akijua angejifungulia nyumbani, lakini hali ikawa tofauti na matarajio.

Flora anasema alipelekwa Mpwapwa alikojifungua mtoto akiwa amekufa, naye akapata matatizo ya kiafya na kulazimika kwenda kutibiwa Kibaha, mkoani Pwani.

Gharama Mpwapwa

Monika Haruna, aliyekwenda kuishi Mpwapwa ili kuwa jirani na hospitali anabainisha maisha ya mjini ni ya aina mbili; kupanga chumba au kukaa eneo la Chigonela.

Monika (31), anasema kwa miaka minane akibeba ujauzito mara tatu amekuwa akihama kwenda kuishi jirani na hospitali ya Mpwapwa.

Anasema mume wake ni mwalimu ambaye humpangia chumba akilipia Sh40,000 kwa mwezi. Anasema ukichanganya na gharama za msaidizi na ununuzi wa mahitaji hufikia zaidi ya Sh300,000.

Kwa wasio na uwezo, anasema huishi eneo lililotengwa na hospitali ambalo ni dogo na mazingira yake si rafiki kutokana na wingi wa watu wanaoishi hapo.

Tiba mbadala

Rose Ngoto (55), tabibu wa tiba mbadala anaeleza kuwa kutokuwapo kituo cha afya au zahanati katika Kijiji cha Kisisi kumemfanya awe na shughuli nyingi za kuwahudumia wagonjwa nyumbani kwake.

Anaeleza kwa kutumia uzoefu wake, amekuwa akiwasaidia hata wajawazito na wengine akiwashauri kwenda kuishi jirani na hospitali.

“Si wajawazito tu, kuna watu wanaopata maradhi mengine tunawatibu na wanapona, mfano mtu akiwa na tatizo la tumbo na homa; hata waliong’atwa na nyoka tunawapa tiba,” anaeleza.

Ushuhuda wa bodaboda

Issa Chidong’oi, dereva wa bodaboda, mara kadhaa amekuwa akibeba abiria na hasa usiku kuwapeleka Mpwapwa.

Anaeleza kuwa ameshawasafirisha wajawazito wanane ambao walijifungua salama, isipokuwa mmoja ambaye mwanawe alikufa siku moja baada ya kuzaliwa.

Dereva huyu ananieleza gharama za kukodi pikipiki wajawazito ni tofauti na wagonjwa wengine; sababu ikiwa ni uangalifu zaidi unaohitajika, pia lazima awe na msaidizi.

Anaeleza kwa kawaida gharama ni kati ya Sh20,000 na Sh25,000 kutoka Kisisi kwenda Mpwapwa, lakini kwa wajawazito huongeza Sh5,000.

Ananieleza wanapotumia barabara ya wajenzi wa reli ya kisasa (SGR) wanapishana na magari makubwa, hivyo ni hatari pia, hukosekana nafasi ya kujificha pale mjamzito anapozidiwa na kutakiwa kujifungua njiani.

Hata hivyo, Dk Elias Kweyamba ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama, anasema kumsafirisha mjamzito aliyeshikwa uchungu kwa mwendo mrefu kwenye pikipiki anakuwa katika hatari yeye na mtoto.

“Kutumia pikipiki si tatizo sana katika maeneo ambayo hayana usafiri mwingine mbadala, hata hivyo umakini unatakiwa kwa kuwa uchungu ukimkolea akiwa safarini hali inakuwa ngumu zaidi, kwa kuwa wanasafiri bila kuwa na mtaalamu,” anasema.

Dk Kweyamba, ambaye anafanya kazi taasisi ya utafiti Ifakara, anashauri wajawazito kuishi jirani na vituo vya kutolea huduma.

Kuhusu tiba mbadala, anasema wanafanya kazi isiyo na utaalamu ambayo wakati mwingine huwachelewesha wagonjwa kufikia huduma mapema.

Nini kinafanyika

Diwani wa kata hiyo, Tano Mkanyago anasema wameanza mchakato wa ujenzi wa kituo cha afya kwa kutenga eneo la ekari 15 na wameshapata matofali 4,100.

“Hii ni kata ya kimkakati, kipindi hiki cha kiangazi ni nafuu kwetu, ikija masika hali ni ngumu mno. Daraja la Godegode ni wimbo wa miaka yote, lakini hakuna kilichofanyika,” anasema Mkanyago.

Anasema endapo kungekuwa na daraja, usafiri kwenda Mpwapwa pasingezidi kilomita 36 kupitia njia ya Kimagai.

Kwa mujibu wa diwani, wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa ya mlipuko ya kipindupindu na homa za matumbo kwa kukosa vyanzo vya maji vya uhakika kwa matumizi ya binadamu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, George Fuime anasema hajui ni lini matatizo yatakwisha kutokana na uwezo mdogo wa mapato ya halmashauri.

Fuime anasema Godegode ni eneo la kimkakati ambalo linawasumbua, licha ya kuwa na uzalishaji mkubwa wa vitunguu.

Anabainisha pia wanakabiliwa na changamoto kwa baadhi ya maeneo yanayozungukwa na milima, ukiwamo mmomonyoko wa udongo; hivyo wanahitaji nguvu ya Serikali Kuu kuyatatua.

Kuhusu barabara, anasema yanahitajika matengenezo makubwa, likiwamo eneo la Godegode ambalo kila mwaka hukumbwa na mafuriko.

Kuna ugumu

Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Mpwapwa, Emmanuel Lukumay anaeleza kuwa ugumu wa matengenezo ya Barabara ya Godegode unatokana na ufinyu wa bajeti.

Lukumay anasema ubovu wa barabara katika Wilaya ya Mpwapwa ni tatizo linalohitaji fedha nyingi, lakini wamekuwa wakitengeneza kwa vipande kulingana na kidogo kinachopatikana.

Anatoa mfano kuwa, bajeti ya mwaka 2022/23 walitengeneza daraja dogo la mfuto eneo korofi la Kijiji cha Kisisi, licha ya ukweli kuwa bado hakupitiki.

Anasema walichonga kilomita nane za barabara kwenye kata ya Godegode na sasa wameelekeza nguvu maeneo mengine.

Katika bajeti ya mwaka huu 2023/24 bila kufafanua, anasema kuna baadhi ya kazi zitafanyika.

Chanzo: mwanachidigital