Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu ya wajawazito wengi kujifungua kwa ‘kisu’

Kujifungua Kwa Njia Ya Upasuaji.png Wanawake kujifungua kwa Kisu

Fri, 20 Aug 2021 Chanzo: MWANANCHI

Imebainika kuwa wapo baadhi ya wanawake wanaoomba kujifungua kwa njia ya upasuaji kutokana na sababu mbalimbali, ukiwamo woga wa uchungu wakati wa kujifungua.

Hayo yameelezwa na wataalamu wa afya baada ya utafiti mpya uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuonyesha ifikapo mwaka 2030 asilimia 29 ya wanawake duniani kote watakuwa wanajifungua kwa njia ya upasuaji.

Utafiti huo umeeleza kwa sasa asilimia 21 ya wanawake wanajifungua kwa njia ya upasuaji na kubainisha kuwa licha ya njia hiyo kuokoa maisha ya wajawazito na watoto, yapo madhara lukuki.

Akizungumzia utafiti huo, Daktari Bingwa wa Wanawake na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Morogoro, Daniel Nkungu anasema licha ya madhara yaliyopo, wapo wanawake wanaochagua kuzaa kwa upasuaji hata kama wanaweza ama wanashauriwa kujifungua kwa njia ya kawaida bila kupata madhara.

“Wanatoa sababu kwamba wanaogopa uchungu wa kuzaa kutokana na hadithi au simulizi wanazozisikia kutoka kwa ndugu au marafiki,” alisema.

Hata hivyo, Dk Nkungu amesema madhara ya kujifungua kwa upasuaji ni mengi, ikiwamo kuathirika kwa ukuta wa mbele wa tumbo, uwezekano wa kupata maambukizi katika njia ya uzazi, maumivu ya kidonda ya muda mrefu na kifo kutokana na athari za dawa za usingizi.

“Iwapo haitafanywa kitaalamu basi madhara yanaweza kujitokeza, wakati mwingine husababisha kilema cha muda mrefu au kifo,” amesema daktari huyo.

Dk Nkungu alisisitiza kwamba “njia ya asili ni salama zaidi.”

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Masuala ya Uzazi na Wanawake, Lawrence Mpangala wa Hospitali ya Ekenywa jijini Dar es Salaam amesema wapo akinamama wanaoomba kujifungua kwa upasuaji wakitoa sababu mbalimbali, ikiwamo kuzaa mtoto katika tarehe sawa na ya baba au ya mama.

“Anakuja mama hapa anaomba ajifungue wa kisu, ukimuuliza sababu anasema mume wangu alizaliwa tarehe hii na mtoto azaliwe tarehe ileile,” alisema.

Dk Mpangala amesema licha ya akinamama hao kuomba kufanyiwa upasuaji, wataalamu huwahoji kupata sababu yenye mantiki.

“Unafika wakati mwanamke analazimisha kufanyiwa upasuaji na inabidi ukubali kwa sababu tayari inakuwa imeshamkaa kwenye mindset (mawazo) na huweza kusababisha akashindwa kuzaa kwa kawaida Ukimkatalia halafu akapata shida kujifungua kawaida, lawama zinakuwa juu yako".

Akizungumzia mtazamo wa wengi kuwa hospitali binafsi huzalisha kwa upasuaji zaidi kwa sababu za kimaslahi, Dk Mpangala amesema yeye huangalia madhara ya upasuaji kuliko fedha.

“Unapofanya upasuaji, unabaki na kovu la milele, una hatari ya kufanya upasuaji katika mimba zijazo,” alisema.

Ingawa uzazi kwa njia ya upasuaji hufanyika ili kuokoa maisha ya mama na mtoto, lakini wataalamu wanasema huweza kusababisha madhara ya muda mrefu kwa mama iwapo hautafanyika kiutaalamu na utafiti huo umeonyesha nchi za Afrika zipo katika hatari.

Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Afya ya Uzazi na Utafiti wa WHO, Dk Ian Askew alisema uzazi kwa njia ya upasuaji ni njia muhimu katika kuokoa maisha, hasa pale njia ya kawaida inaposhindikana, hata hivyo si kila ‘C-Section’ inafanyika kwa sababu za kitabibu.

“Upasuaji bila sababu unaweza kusababisha madhara kwa mama hata mtoto,” alisema.

Kwa mujibu wa WHO, kuzaa kwa upasuaji kunasababishwa na unene kupita kiasi, au mtoto kuwa mkubwa kuliko nyonga ya mama.

“Zamani wanawake walikuwa wakizaa watoto wenye kilo 2.2 au 2.5, lakini siku hizi mtoto anaweza kuwa kilo 3.8 hadi tano wakati mwingine, kwa hali hii ni vigumu kuzaa kwa njia ya kawaida,” alisema Dk Nkungu.

Amesema mtindo wa maisha unachangia watoto kuwa wakubwa wakiwa tumboni, kwa mfano kutofanya mazoezi, ulaji mbaya hasa wa vyakula vya sukari iliyolainishwa.

Sababu nyingine ni ukuaji wa teknolojia ambapo ni rahisi kujua changamoto alizonazo mama kabla hajajifungua kwa kutumia mashine ya ‘ultra sound’, hivyo wataalamu kujua iwapo upasuaji utahitajika au la, tena kwenye hatua za awali kabisa.

“Elimu imepanuliwa zaidi na sasa wataalamu wa afya wanatakiwa kuweka umuhimu zaidi katika kuokoa maisha ya mama na mtoto, hivyo tunapoona kuna hatari, mara moja tunafanya upasuaji,” alisema Dk Nkungu.

Amesema sababu nyingine ya ongezeko la upasuaji ni kutokana na wengi kuzaa katika umri mkubwa kutokana na mitindo ya kimaisha, ikiwemo elimu na ajira.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi wa Hospitali ya Salaamani iliyopo Temeke, Dk Abdul Mkeyenge anasema wanawake wanachagua kujifungua kwa upasuaji kwa fikra zao wenyewe na wao kama madaktari hawashauri jambo hilo, ila ni kwa sababu maalumu ambazo mjamzito anaweza kuwa nazo.

Anazitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni kupata uchungu lakini mtoto kutotoka, mtu aliyebeba mimba ya watoto pacha ambao wamekaa vibaya, shinikizo la damu la juu, presha ya kupanda ambayo inasababisha kupata kifafa cha mimba pamoja na mimba kufikia kipindi cha kujifungua, lakini mtoto amegeuza makalio.

“Ndio maana kuna saa maalumu ya uchungu, kwa hiyo ikipitiliza inaweza ikachangia mtoto kupata matatizo. Kwa hiyo tunalinda afya ya mama na mtoto ndio maana inatakiwa afanyiwe upasuaji.

“Mtu ambaye alizaliwa kwa upasuaji unaweza ukampa saa kadhaa ya kusukuma, lakini ikishindikana itabidi afanyiwe tena upasuaji ili asije akapata madhara.

“Kwa hiyo sio kwamba madaktari wanapenda kuwafanyia watu upasuaji, ila inatokana na viashiria ambavyo vitajitokeza,” anasema Dk Mkeyenge.

Anafafanua kuwa sio kwamba watu wengi siku hizi wanafanyiwa upasuaji, ila zamani ilikuwa kati ya wajawazito 10,000 ni wajawazito 450 wanafariki kutokana na changamoto za uzazi kwa mwaka.

“Lakini kwa sasa hivi ukija kuangalia hizi takwimu zinapungua, vifo vya uzazi vimepungua na hii ni kutokana na Serikali kujitahidi kuweka vituo vingi vya afya na vitendea kazi vya kutosha,” anasema Dk Mkeyenge. Hata hivyo, anatoa wito kwa Serikali kuzidi kutanua vituo vya afya na endapo mtu akijigundua ni mjamzito anatakiwa aanze kliniki katika wiki 12 za kwanza.

Mkunga mbobezi jijini Dar es Salaam, Feddy Mwanga anabainisha kuwa mjamzito anayependa kujifungua kwa upasuaji anaweza kupata ulemavu wowote unaoingilia maumbile ya nyonga.

“Pia mwanamke akiwa na kimo kidogo anakuwa na nafasi kubwa ya kujifungua kwa upasuaji, ndio maana tunawaambia ukijiona una kimo kidogo ujitahidi kuwahi kituo cha afya,” anasema.

Judika Losay, Mwanachama wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) amesema ukuaji wa teknolojia ya afya unasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Neema Msangi, mkazi wa Kibaha amesema: “Wanaogopa kuharibu njia zao ndiyo maana wanachagua kisu, hayo ndiyo tunayoyasikia kutoka kwa wenzetu.”

Chanzo: MWANANCHI