Baadhi ya madaktari na wakunga wamesema huduma inayotolewa na wafanyakazi wa kada za afya vituoni huenda ikawa ni sababu inayowafanya wanawake kuhama hospitali pindi wanapotaka kujifungua.
Hayo yamesemwa Septemba 17, 2021 wakati wa maadhimisho ya siku ya usalama wa mgonjwa duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Aga Khan.
“Moja ya vitu vya msingi kuvizingatia ni namna unavyotoa huduma kwa mama mjamzito na mtoto mchanga, usiache nafasi kosa lolote likatokea na hilo ndilo linalomfanya mgonjwa atamani kurudi tena na tena, pia huduma huwa inakwenda vizuri kwani mgonjwa pia anatoa ushirikiano” amesema Mkuu wa Kitengo cha uzazi na magonjwa ya kinamama Hospitali ya Aga Khan, Dk Munawar Kaguta.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi Tanzania (AGOTA) ambao wamesema kitengo cha afya ya mama na mtoto ni sehemu ya kupambana ili kuokoa maisha.
“Ukiwa kwenye hii idara ni kujituma ili mtoto na mama wote wawe salama, huko nyuma tuliwapata wajawazito kwa asilimia 40 lakini takwimu zinatuonyesha kuwa mpaka sasa tumefanikiwa asilimia 63 ya kinamama wanajifungulia vituoni, inabidi tutie bidii kuwapata wote.
“Tujiulize kwanini mama apime kwako akajifungulie sehemu nyingine au nyumbani. Wana fikra nyingi zinazowafanya wasije kwetu, kuna vitu vyao tupende kuvijua vinavyowafanya wasije kwetu, tuzidishe utu, kuwajali na ukarimu,” amesema Rais wa AGOTA, ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Matilda Ngarina.
Mkuu wa kitengo cha viwango na usalama wa wagonjwa Aga Khan, Nyangee Lugoe amesema , “Lengo ni kuhakikisha usalama wa mgonjwa unazingatiwa na hospitali hiyo inafanya kazi kwa malengo makubwa ya kuhakikisha inaokoa maisha kwa huduma zenye viwango na usalama kwa mgonjwa.”
Akitoa ushuhuda mtangazaji maarufu ambaye pia ni mwanahabari, Zamaradi Mketema amesema aliwahi kuondoka katika moja ya hospitali kwa kuwa tu hakurudhishwa na huduma akiwa mjamzito.