Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu wagonjwa wa fistula kupungua

Fistula 3000 Sababu wagonjwa wa fistula kupungua

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dodoma. Kusogezwa kwa huduma za afya kuanzia ngazi za chini kumesaidia kupunguza idadi ya wanawake wanaopata ugonjwa wa fistula, ambao unasababishwa na mama mjamzito kukosa huduma ya haraka kutokana na kupata uchungu pingamizi.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana Jumapili Januari 21, 2024, daktari bingwa wa magonjwa ya kike na uzazi kutoka Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma General, Abed Ikwasa, amesema idadi ya kina mama wanaopata ugonjwa huo imepungua tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Dk Ikwasa amesema ugonjwa wa fistula unatokana na mama mjamzito kupata uchungu pingamizi kwa muda mrefu bila kujifungua na hivyo kusababisha kupata tundu linalounganisha mfumo wa mkojo na uke au njia ya haja kubwa na uke.

Amesema linapotokea tatizo hilo, mama anashindwa kuzuia haja ndogo au haja kubwa na hivyo kuanza kutoka yenyewe na kama asipopata matibabu ya haraka, anaweza kubaki hivyo maisha yake yote.

Dk Ikwasa amesema hivi sasa idadi ya akina mama wanaopata ugonjwa huo imepungua kutokana na serikali kusogeza huduma za afya na matibabu ya kibingwa ikiwemo madaktari wa upasuaji hadi ngazi ya vituo vya afya.

Amesema hivi sasa huduma imesogezwa tofauti na zamani ambapo vituo vya afya vilikuwa ni vichache na hivyo kusababisha wanawake wengi wajawazito kukosa huduma za afya kwa haraka na hivyo kusababisha wengi kupata ugonjwa wa fistula.

“Hivi sasa kuna huduma ya upasuaji kwenye vituo vya afya, hivyo hata kama mama atapata uchungu pingamizi, akifikishwa kwenye vituo vya afya atafanyiwa upasuaji bila shida yoyote kwa sababu wataalam wameshushwa hadi huko chini,” amesema Dk Ikwasa na kuongeza:

“Na ndiyo maana tunaona idadi ya wagonjwa wa fistula imepungua kwa sababu kina mama wajawazito wanapata huduma kwa wakati tofauti na zamani walipokuwa wanafunga safari hadi hospitali ya mkoa ambapo walikuwa wanafika wameshachelewa.”

Mtaalam huyo amesema kwa mwaka 2023, hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na hospitali ya CCBRT ilifanya kampeni maaluma ya kuwatafuta wanawake wenye ugonjwa huo, ambapo walipata jumla ya kina mama 35 ambao walikuwa na ugonjwa huo.

Amesema kati yao, 32 walipatikana maeneo mbalimbali nchini na watatu ndiyo walifika wenyewe hospitalini hapo kupata huduma baada ya kujua kuwa wamepata ugonjwa huo.

Amebainisha kuwa chanzo cha wanawake wengi wajawazito kupata ugonjwa huo ni kuchelewa kupata huduma ya kujifungua pale wanapopata uchungu pingamizi, hali inayosababisha mtoto kuchelewa kutoka na hivyo kumsababishia mama madhara.

“Sasa hivi hata miundombinu ya barabara huko vijijini imeboreshwa na zinapitika katika kipindi chote cha mwaka, hivyo hata kama mjamzito atashindwa kupata huduma kwenye ngazi za chini atafikishwa kwa haraka hospitali ya rufaa kwa sababu barabara zinapitika kirahisi,” amesema Dk Ikwasa.

Ili kujikinga na ugonjwa huo, Dk Ikwasa ameshauri kina mama wajawazito kuhudhuria kliniki mara tu wanapojijua kuwa wameshika mimba ili kama kutakuwa na changamoto zozote zitakazoonyesha hawezi kujifungua kawaida wazitatue mapema.

Daktari huyo amesema zipo sababu nyingine zinazoweza kusababisha mama kupata ugonjwa huo nje ya kujifungua kama vile ajali, maambukizi ya magonjwa, saratani ya shingo ya kizazi, kuharibika kwa mimba au kutoa mimba na wakati wa upasuaji.

Ili kujikinga na ugonjwa huo, Dk Ikwasa ameshauri kina mama kubeba mimba wakiwa na miaka 20 au zaidi na kuwahi kufika kwenye vituo vya afya pindi wanaposikia uchungu wa kujifungua ili wapate huduma bora.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live