Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SUA watakiwa kushirikiana na tiba asili tafiti za corona

24bd8f6c46edab45f3dd0f95bf2ae37a.jpeg SUA watakiwa kushirikiana na tiba asili tafiti za corona

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATAALAMU wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kushirikiana na wataalamu wa tiba asili, tiba mbadala na taasisi nyingine katika kufanya tafiti za dawa ambazo zitasaidia dunia kupambana na ugonjwa wa covid-19 unaotokana na virusi vya corona na magonjwa mengine hatari kwa binadamu, wanyama na mimea.

Rai hiyo imetolewa kutokana na takwimu za hapa nchini kuonesha kuwa tiba asili na tiba mbadala zina mchango wa zaidi ya asilimia 45 katika matibabu na kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Paul Mhame alitoa wito huo wakati wa ufunguzi wa jukwaa la ubunifu la wadau wa tiba asili Tanzania uliofanyika Chuo Kikuu cha SUA mkoani Morogoro juzi.

"Upatikanaji tiba asili na tiba mbadala zinazotokana na mimea itasaidia kufikia wananchi wengi hasa wanaoishi vijijini," alisema.

Dk Mhame alifafanua biashara ya tiba asili duniani inakuwa kwa kasi kwani kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2000 mauzo yake yalikuwa dola za Marekani bilioni 20, mwaka 2012 yalipanda na kufikia dola za Marekani bilioni 60 na mwaka 2018 yalifikia dola bilioni 80.

Alisema kutokana na umuhimu wake, ndio maana serikali imetunga sheria ya tiba asili na tiba mbadala namba 23 ya mwaka 2002.

Alisema inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 mauzo ya dawa za asili na tiba mbadala yatafikia dola za Marekani trilioni tatu.

"Kwa hiyo niwaombe watafiti wa SUA na waganga wa tiba asili nchini kushirikiana ili kusaidia kujipanga vizuri Tanzania nayo inufaike kama China na nchi zingine duniani kwenye mauzo ya dawa za tiba asili," alisema.

Naye Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko aliwataka waganga wa tiba asili na tiba mbadala kuendelea kushirikiana na ofisi yake katika kupima viambata mbalimbali vinavyopatikana kwenye dawa zao ili kusaidia kuepusha madhara yoyote yanayoweza kutokea kwa wateja wao endapo dawa itakuwa na viambata ambavyo sio salama.

"Kazi ya ofisi yangu sio kuzuia nyinyi kupata usajili wa dawa zenu bali tunataka kuona kila dawa mnayoitoa kwa wagonjwa iwe na viambata sahihi ili iweze kutibu vizuri na isilete madhara kwa wateja wenu, lakini pia upimaji wetu ndio wa mwisho ili muweze kupata usajili wa dawa tukiweka sahihi yetu kuwa dawa iko salama hakuna wa kupinga hivyo msiogope tushirikiane,” alisema.

Dk Mafumiko alikipongeza chuo hicho na watalaamu wake kwa jitihada wanazofanya katika kuwasaidia waganga wa tiba asili waweze kuboresha huduma ya tiba wanazotoa kwa jamii ili ziwe na viwango vinavyohitajika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mradi wa Uvumbuzi katika Mimea Dawa kwa Ustawi wa Watanzania (GRILI), Dk Faitha Mabiki alisema kumekuwa na mafanikio makubwa kwa wadau wa tiba asili nchini na wanashirikiana na wataalamu wa sekta hiyo kuhakikisha biashara ya tiba asili na mimea dawa inachangia uchumi wa wadau hao na taifa.

"Wakati tunaanza mradi huu mwaka 2018 waganga wengi wa tiba asili walikuwa wanauza dawa zao kwenye mifuko ya rambo, magunia na vifungashio vingine visivyo na ubora, lakini tunafurahi leo wakati tunazindua jukwaa hili tunaona wote wameweka dawa kwenye vifungashio bora na vyenye viwango vinavyokubalika kitaalamu," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz