WATAFITI wa Idara za Kemia na Fizikia katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamepongezwa kwa juhudi wanazofanya kuwajengea uwezo waganga wa tiba asili na tiba mbadala ili kuongeza thamani ya dawa zao na matumizi endelevu ya miti.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk David Ntahindwa, alitoa pongezi hizo hivi karibuni mjini Njombe wakati akifungua mafunzo kwa waganga hao wa tiba asili na tiba mbadala wa Mkoa wa Njombe.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na SUA kupitia Mradi wa Uvumbuzi katika Mimea Dawa kwa Ustawi wa Watanzania (GRILI) kwa kushirikiana na mradi wa kuongeza thamani kwa kemikali za SG kwa matibabu ya magonjwa ya binadamu na wanyama (vaSPHAD).
Dk Ntahindwa alisema katika kipindi cha hivi karibuni, dawa asili na tiba mbadala zimepata umaarufu kutokana na watu wengi kuanza kuzitumia kutibu magonjwa mbalimbali.
Alisema pamoja na matumizi hayo, bado mazingira ya utengenezaji wake na matumizi hayawekwa sawa ipasavyo hali inayowafanya watu wengi kusita kuzitumia kwa kuhofia usalama wao.
"Mafunzo haya yanayoendeshwa na watafiti wa SUA yataongeza thamani ya dawa hizi na kuhakikisha usalama watumiaji, kwani mtazingatia kanuni bora za utengenezaji na ufungashaji ili kutoa tiba inayokusudiwa," alisema.
Alisema mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi ambapo serikali inasisitiza na kuzipa kipaumbele dawa za asili ili kutibu magonjwa yanayoweza kutibika na dawa hizo, badala ya kutegemea dawa kutoka nje ya nchi wakati zinatoka kwenye miti na mimea iliyopo nchini.
Mkuu wa mradi wa GRILI, Dk Faith Mabiki alisema umefika wakati kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala kunufaika na kazi zao wanazozifanya kwa kutoa huduma bora za matibabu na wao wenyewe kujiongezea kipato kwa kutanguliza utu.
Alisema hilo litawezekana endapo waganga hao wataongeza thamani ya dawa zao na kushiriki kulima miti dawa hiyo ili isipotee kwa kuwa kwa sasa wanaivuna kila siku.
Hivyo, alisema kuna dawa nyingi zinatoka nje ya nchi hasa China na kutibu watu huku zikiwa zimeboreshwa, lakini miti iliyotumika pia ipo hapa nchini.
"Sasa wakati umefika dawa zetu ziongezwe thamani na kuuzwa kwa wingi nchini na nyingine kuzisafirisha kwenda nje ya nchi na mafunzo haya yatawasaidia kuongeza thamani kwa kuzifungasha vizuri, kuziwekea taarifa muhimu za kemikali zilizo kwenye dawa na namna ya kuzitumia na hivyo kuinua kipato chenu na cha taifa,” alisema Dk Mabiki.
Dk Mabiki, alisema kwa kuwa mahitaji ya miti dawa yanaongezeka siku hadi siku, upo uwezekano wa miti mingi kupotea hivyo ni muhimu waganga hao kuanza kulima kilimo cha miti dawa na mimea dawa ambayo ni muhimu kutoa tiba na kurahisisha upatikanaji wake.
Kwa mujibu wa mkuu wa mradi huo, waganga wa tiba asili na tiba mbadala zaidi ya 20 na viongozi wao wa wilaya zote za Mkoa wa Njombe walifundishwa kanuni za msingi za usindikaji wa dawa, athari za usugu wa dawa, kemikali zinazopatikana kwenye mimea dawa nchini na namna ya kupanda mimea dawa hiyo katika mashamba na kustawisha.