Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Mwinyi: Tutajenga hospitali kubwa mbili za wajawazito

IMG Hospital Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wanatarajia kujenga hospitali kubwa mbili za wajawazito kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo na kuwaondolea adha wanayopata.

Iwapo hospitali hizo zitajengwa zitapunguza adha hiyo hususani katika hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja ambayo inaonekana kuelemewa. Kwasasa katika wodi ya wazazi kitanda kimoja kinalaliwa na wanawake hadi watano.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo jana Juni 11, 2023 alipokuwa akizungumza na mabalozi na wajumbe wa Halmashauri ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati akihitimisha ziara yake ya kichama katika mikoa ya Unguja.

Bila kutaja lini zitaanza kujengwa na kiasi cha fedha kitakachotumika, Dk Mwinyi amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo inawataka kuleta huduma nzuri kwa wananchi wake.

"Watu wengi wanapokwenda hospitali katika kitengo cha uzazi mara zote kunakuwa kumefurika hivyo tumeona kuna umuhimu wa kujenga hospitali hizo, moja itakuwa katika Wilaya ya Mjini na Hospitali ya Mwembeladu itafanyiwa ukarabati mkubwa," amesema.

Kuhusu sera ya utoaji wa huduma bure kisiwani hapo, Dk Mwinyi amesema bado ipo palepale ingawa kumekuwapo na maboresho mbalimbali lengo ni kuwapatia huduma bora wananchi.

Amesema wataendelea na mpango wa kuzishirikisha sekta binafsi katika utoaji wa huduma hizo ili kuleta ufanisi mkubwa zaidi huku akidai wapo baadhi ya watu kupotosha ukweli kuhusu ushirikiano huo.

"Malipo yote yatafanywa na serikali na sio kutolewa na mwananchi hivyo, wananchi puuzeni hizo propaganda zinazotolewa kuwa eti mtalipa huduma zitakazotolewa katika vituo vya afya," amesema.

Pia amesema watajenga hospitali kubwa ya kisasa katika eneo la Binguni ili wananchi wapate huduma bora kisiwani humo bila kufuata huduma hizo nje ya Zanzibar.

Akizungumzia kuhusu ziara hiyo, Dk Mwinyi amesema lengo ni kukumbushana wajibu wao kama chama na kujua changamoto inazowakabili viongozi hao kuanzia ngazi ya shins hadi mkoa.

Amesema baada ya uchaguzi wa chama kumalizika zipo kasoro zilizotokea kwa sababu ya makundi hivyo ni vyema kuachana na makundi hayo ili kukipa ushindi chama wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

"Tunajua kuwa yapo makundi kwani kina kila aliyemtaka lakini inavyotakiwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi baada ya viongozi wameshachaguliwa basi sote tuvunje kambi zetu na tuwe nyuma ya wale waliochaguliwa," amesema.

Hivyo, aliwasisitiza kuvunja makundi hayo na kukijenga chama na kufanya kazi inayowakabili ya kukiletea chama cha CCM ushindi wa mwaka 2025.

Alisema kazi ya kwanza ya chama cha siasa ni kushika dola, hivyo wanaCCM wanawajibu wa kujiandaa kwa mwaka 2025 kushika dola.

Hivyo, amesema ili kufanikisha hilo wataandaa mafunzo kwa ajili ya viongozi waliochaguliwa kwa ngazi zote ili kuona wanaengeza wanachama.

"Tutatafuta uwezeshaji ili tuone kila kiongozi anajua wajibu wake kuanzia ngazi za chini kuanzia shina hadi mkoa ili kutambua wajibu wake," amesema.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Mohamed (Dimwa), amesema ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Dk Mwinyi wamepiga hatua kubwa za maendeleo na kumtaka aendelee kutekeleza ilani bila kuvunjika moyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live