Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Magufuli ampa pole Dk Kigwangalla

10157 PIC+MAGGUU TanzaniaWeb

Sun, 5 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amempa pole Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliyepata ajali ya gari leo Jumamosi Agosti 4, 2018 mkoani Manyara na kupata majeraha sehemu mbalimbali mwilini.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inasema kiongozi mkuu huyo wa nchi amemuombea waziri huyo apone haraka na kuwashukuru madaktari na wauguzi wa kituo cha afya Magugu walioanza kumpa huduma ya kwanza.

Pia, amewashukuru viongozi  wa hospitali ya Selian ya jijini Arusha kwa juhudi walizozifanya kuokoa maisha ya Dk Kigwangalla na majeruhi wengine wa ajali hiyo.

Rais Magufuli ametoa salamu za pole kwa familia, wafanyakazi wa wizara, ndugu, jamaa na marafiki wote kufuatia kifo cha ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa leo jioni Rais Magufuli aliungana na viongozi wa wizara hiyo kumpokea Dk Kigwangalla katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Dk Kigwangalla amesafirishwa kwa ndege kutoka Arusha kuja jijini hapa kwa matibabu zaidi.

Inaeleza kuwa waziri huyo amepata ajali katikati ya vijiji vya Mdolii na Minjingu Wilaya ya Babati mkoani Manyara baada ya gari lake kupinduka na kusababisha kifo cha Temba huku watu wengine watano akiwemo yeye kuumia.

Akiwa JNIA, Rais Magufuli alikuwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya.

Chanzo: mwananchi.co.tz