Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RIPOTI MAALUMU: Kuweka rehani utu, uhai kwa ajili ya usafi wa wengi

84799 Pic+usafiri RIPOTI MAALUMU: Kuweka rehani utu, uhai kwa ajili ya usafi wa wengi

Tue, 19 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika eneo la Kisutu jijini Dar es Salaam, namuona mfagiaji akisukuma tolori la taka kuelekea kwenye jalala dogo linalohifadhi taka kwa muda.

Ghalfa gari inakanyaga dimbwi kubwa kisha maji machafu yanamrukia mfagiaji huyo na kumlowanisha upande wake wa kulia wa mwili.

Nguo za mama huyo anayeitwa Lucy Kisenga mwenye umri wa kati ya miaka 55 hadi 60 zinalowana.

Atafanyaje! Analigeukia gari lililomwagia maji ambalo dereva wake hajali kilichotokea, anatikisa kichwa na kuanza kujifuta baadaye kuendelea na safari yake. Alikuwa ameshakamilisha kazi katika kipande chake majira ya saa 2:00 asubuhi.

“Ni kawaida mwanangu, tumezoea hali hii,” anasema baada ya kumpa pole.

“Unajua madereva wengi wanaangalia kuwahi wanakoendatu, hawajali kama kuna watu wengine wanaotumia barabara. Wanaona sisi wafagiaji kama hatuna maana kabisa.”

Kisenga ni mmoja kati ya wafanyausafi jijini Dar es Salaam, wengi wao wakiwa ni wanawake, ambao wanafanya kazi hiyo katika mazingira magumu, wakiweka hatarini maisha yao, afya, usalama, staha na utu wao.

Na bado malipo yao, hayaakisi kazi kubwa wanayoifanya na pengine ndio maana vijana wa jinsi nyingine hawashawishiki kujiunga nao.

Kisenga anasema kazi hiyo ingekuwa na maslahi mazuri, makundi mengine yangeingia kuifanya.

Mwananchi ilifuatilia eneo la kituo cha mabasi cha Ubungo (UBS), ambacho kina harakati nyingi za wasafiri na wafanyabiashara kujua utendaji kazi wa wafanyakazi hao.

Akinamama hao huonekana katika barabara nyingi kubwa za jiji la Dar es Salaam wakiwa wamejifunika khanga mwilini, vilemba kichwani na baadhi wakiwa wameweka kifaa cha kuzuia vumbi kuingia mdomoni na puani.

Wengi hawana glovu za kuwaepusha kushika taka wanazokusanya na mifagio yao ni ile iliyotengenezwa kwa ajili ya matumizi ya majumbani na si eneo kubwa la barabara.

Vifaa vyao hivyo vinaonyesha dhahiri kuwa ufanisi wa kazi yao ni mdogo na hivyo si rahisi kuondoa mchanga kikamilifu eneo analopangiwa zaidi ya kutimiza wajibu.

Lakini kilicho kibaya ni usalama wao.

Si jambo la ajabu kuona dereva akimpigia honi mfagiaji ili ampishe badala ya kufuata alama aliyowekewa ya kutakiwa apite pembeni.

“Hata ukiweka alama kwamba unafanya usafi, wengine hawajali. Anaweza kukupitia miguuni, hivyo huwa tunapisha,” anasema Kisenga.

Mwananchi ilishuhudia mmoja wao akikimbia kukwepa gari lililokuwa linamfuata kwa kasi sehemu aliyokuwa akifagia eneo la Sinza Mori.

Akionekana kuudhika, alikwenda kukaa pembeni kutafakari.

Na hatari kama hiyo ni ya kawaida kwa wafanya usafi hao kama anavyosema Bethelina Kihaka wa eneo la stendi ya Ubungo.

“Inabidi tusubiri mabasi yanayotoka saa 12:00 asubuhi yaondoke kabisa ndio tuanze kufagia vinginevyo unaweza kugongwa. Bila umakini ni hatari sana,” alisema.

Kushushwa utu

Hatari ya kudhurika si adha pekee wanayokumbana nayo wafanya usafi hao. Kupewa majibu mabaya, kutukanwa na kudhalilishwa ni tatizo jingine kwa watumishi hao wa umma na sasa mambo hayo ni sehemu ya maisha yao.

Katika eneo la mabasi Ubungo, kijana aliyekuwa akila embe alitupa mabaki eneo ambalo lilishafagiliwa.

“We kijana okota hilo kokwa katupe kwenye dustbin (pipa la taka), si ile pale? Kwa nini unatupa hapa wakati nimetoka kufagia?” alisema mama aliyekuwa akifagia eneo hilo ambaye baadaye alijitambulisha kwa jina la Bethelina Kihaka.

“Achana na mimi we mama! Si umeajiriwa kwa kazi hiyo? Okota mwenyewe,” alijibu kijana huyo huku akiondoka.

Sauti kali ya kijana huyo ilimfanya Bethelina atulie na kuendelea na kazi yake.

“Nafagia stendi mwaka wa kumi sasa kwa hiyo hayo ya kujibiwa vibaya ni kawaida. Tunapambana nayo kila siku,” alisema Bethelina.

Ofisa Afya wa Stendi ya Ubungo, Bahati Godi anakiri watu wanaofanya usafi hawathaminiwa licha ya umuhimu jukumu hilo.

“Niliwahi kuona mtu akimjibu vibaya mfanyausafi. Nilimkamata nikamchukulia hatua. Huyu alitupa takataka hovyo akijua wazi eneo hilo limesafishwa na kuna chombo cha kuwekea taka zake,” alisema Bahati.

“Hii ni changamoto na ndio maana wasichana au vijana wadogo hawapendi kufanya kazi hii, inaonekana ya watu fulani tu.”

Mshauri wa mazingira mkoani Dar es Salaam, Dk Churchill Mujuni anasema wanaofanya usafi wanapaswa kuheshimiwa kama wafanyakazi wengine kwa sababu wanafanya mazingira yawe safi.

“Hawa wanaowapigia honi na kutupa uchafu wanapoona kuna mtu anafagia ama hawajali au hawajui umuhimu wa kazi ya hawa watu, hili ni tatizo,” anasema Dk Mujuni.

Watumishi hawa wa umma pia wanahatarisha maisha yao kutokana na kutokuwa na vifaa sahihi vya usafi.

Dk Kilawa anasema kwa sababu hiyo wapo hatarini kuugua magonjwa ya ngozi, kuhara, macho na mfumo wa njia ya hewa.

Magonjwa mengine ni kifua kikuu, mafua na magonjwa ya mlipuko kulingana na mazingira yao ya kazi.

Dk Kilawa anasema kwa sababu ya umaskini wengi wanashinda kazini bila chakula na hata wakila sio, chakula bora kinachotakiwa kwa ajili ya kujenga mwili.

“Kama ana kipato kidogo anaweza kushinda kazini bila chakula na akirudi nyumbani anakutana na chakula kisicho mlo kamili. Hawezi kupata maziwa kila siku kwa sababu ya kazi yake, hii ni hatari,” anasema na kuongeza;

“Watu hawa muhimu kwa jamii yetu wanatakiwa kusaidiwa ili thamani ya kazi yao ionekane kwa sababu wanashughulikia mazingira yetu tunayoishi kila siku,” anasema Dk Kilawa.

Uchafu uliokithiri

Katika eneo la stendi kuu ya mabasi Ubungo, wafagiaji huokota chupa ambazo baadhi huwa na haja ndogo.

“Kawaida dada yangu. Kuna wakati unakutana na kinyesi. Yaani mtu anajisaidia halafu anatupa,” anasema mfagiaji, Salma Kangi.

“Inabidi uokote na kwenda kutupa jalalani.”

Bahati, anasema kwamba licha ya kuwepo sheria zinazowabana watu bado wanajisaidia na kutupa hovyo uchafu huo.

“Hapa stendi kuna mchanganyiko mkubwa wa watu. Kuna wanaoelewa kuhusu usafi na wasioelewa. Kuna wengine wanaelewa lakini hawajali kwa hiyo kila mtu ana hulka yake,” anasema Bahati.

Anasema huwa wanatumia sheria ndogo za jiji kudhibiti mazingira hata hivyo, si wakati wote wanaweza kukatama wachafuaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz