Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RIPOTI MAALUMU: Jinsi bidhaa zilizotupwa dampo zinavyorudishwa sokoni Dar-1

36720 Pic+dampo RIPOTI MAALUMU: Jinsi bidhaa zilizotupwa dampo zinavyorudishwa sokoni Dar-1

Wed, 16 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni wazi kwamba kama ulikuwa hujui juu ya taka hizo kurejea mitaani, sasa una kila sababu ya kutumia umakini wa ziada unapoamua kununua bidhaa katika maeneo rasmi na yasiyo rasmi usije ukajikuta unanunua bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi.

Uchuguzi uliofanywa na Mwananchi kwa zaidi ya mwezi mmoja umebaini kuwa baadhi ya vyakula na bidhaa nyingine zilizokwisha muda ambazo hutupwa kwenye dampo la Pugu Kinyamwezi, Dar es Salaam hurudishwa sokoni na kuuzwa kama bidhaa mpya.

Gazeti hili limebaini kuwa biashara biashara hiyo ni kubwa na ina mtandao mkubwa ambao vinara wake wamefikia hatua ya kumiliki maghala kwa ajili kuhifadhi bidhaa hizo. Katika maghala hayo bidhaa hizo hupakiwa upya kwenye mifuko au vyombo vingine na inapobidi hugongwa mihuri ili kuwalaghai walaji kuwa muda wa matumizi yake haujapita.

Mbali na bidhaa zilizopita muda zinazotoka Kinyamwezi, Mwananchi limegundua kwamba vinara wa biashara hiyo huzichukua ‘juu kwa juu’ bidhaa hizo kabla ya kufikishwa dampo kuteketezwa na kuzihifadhi katika majumba ama maghala yao. Katika maeneo hayo bidhaa hizo hugongwa mihuri mipya na kuwekewa ‘lebo’ mpya na kisha hurudishwa sokoni.

Bidhaa zafukuliwa

Mwananchi limebaini kuwa vijana wanaotumiwa na vinara wa biashara ya vyakula na bidhaa hizo huingia dampo usiku wa manane na kufukua kwa kutumia majembe na mikono vitu vinavyofikishwa na kuteketezwa chini ya ulinzi.

Baada ya kufukuliwa, bidhaa hizo husafishwa na kisha kufanyiwa utaratibu wa kurudishwa sokoni na kuuzwa ‘kiujanjaujanja’ pembezoni mwa barabara na hata kwenye maduka.

Bidhaa hizo ni pamoja na unga wa ngano, mahindi, mchele, maziwa ya unga, kahawa, majani ya chai, pampasi za watoto, dawa za meno, sabuni, aina mbalimbali za mafuta ya kupaka na vipodozi.

Zimo pia pipi, chokoleti, biskuti, mafuta ya kupikia, taulo za kike, saruji, vinywaji vikali kama bia, mvinyo pamoja na nyama, samaki, tambi na sukari.

Ghala ndani ya dampo

Ndani ya dampo la Kinyamwezi, kwa mfano, kuna ghala linalomilikiwa na mmoja wa vinara wa biashara hiyo aliyetajwa kwa jina la Elias.

Kinara huyo anadaiwa kumiliki leseni ya kuchukua bidhaa zilizokaa muda mrefu na zilizokwisha muda wa matumizi kutoka Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengine kwa lengo la kuzalisha taka rejea.

Mwananchi limegundua kuwa kuna bidhaa toka katika ghala hilo ambazo hurudishwa sokoni.

Mwandishi wetu aliweka kambi eneo la dampo la Kinyamwezi na kujifanya mnunuzi au mlanguzi wa bidhaa ziliyokwisha muda wa matumizi.

Pale alishuhudia, alielezwa na wakati mwingine kuuziwa bidhaa hizo na mawakala pamoja na vinara wa biashara hiyo.

Ndani ya ghala la Elias alipokewa na vijana wanne, mmoja akiwa ndiye mlinzi mkuu aliyemweleza kuwa ni kweli wao huhifadhi bidhaa toka dampo ambazo huuzwa toka pale.

“Ni kweli tunauza lakini bosi mwenyewe hayupo, kama utaweza nenda halafu urudi saa saba mchana maana amesema yuko njiani anakuja, si unaona kuna mzigo wa Vita Malt uliletwa jana bado haujachukuliwa,” alisema mmoja wa vijana hao wa Kimasai, huku akionyesha lundo la vinywaji hivyo.

Aliporudi saa saba mchana, mwandishi wetu hakumkuta mmiliki wa ghala hilo, lakini alipokaribishwa ndani ya ghala hilo safari hii alishuhudia bidhaa kadhaa zikiwa katika malundo mawili ya tambi, pipi, chokoleti, Vita Malt pamoja na mahindi ya njano zikiwa zimehifadhiwa kwenye magunia.

“Ni kweli hapa ukitaka bidhaa za aina yoyote utapata, lakini bosi hajarudi alisema atafika saa saba, lakini hajafika labda cha kukusaidia chukua namba yake utawasiliana (naye) kwa simu, mzigo bado upo,” alisema kijana mwingine huku akimkabidhi ‘zawadi’ ya kinywaji kilichoisha muda na kumtaka akifiche.

Juhudi za kukutana na mmiliki wa ghala hilo hazikuzaa matunda. Hata hivyo, alikiri kwa njia ya simu kuwa ni kweli anafanya biashara hiyo isipokuwa alikuwa amesimama kwa muda huku akiahidi kumtaarifu mwandishi pindi atakapoanza kazi.

“Ni kweli tunafanya hiyo biashara ila kwa sasa tumesimama kwa muda kidogo, kwani ulikuwa unataka mzigo gani?” alihoji.

Mwandishi wetu alimweleza anahitaji tambi ambapo alimjibu, “Sawa kwa kuwa nina namba yako nitakujulisha.”

Askari wa upelelelezi (jina tunalo) anakiri kumfahamu kinara huyo wa biashara za dampo akidai ni mtu anayekwepa mitego wanayomwekea ili kumkamata.

“Nimeshajaribu kutafuta namna ya kumkamata lakini naishia kufeli, pengine unaweza kutusaidia kutupa taarifa za kina ili akamatwe,” alisema askari huyo katika mazungumzo na Mwananchi.

“Inasemekana huyu jamaa yuko idara nyeti (anaitaja) lakini hatujapata ushahidi kamili wa shughuli yake. Lakini huwa ninajiuliza kama ni mtu wa (anaitaja tena idara hiyo) mbona anafanya kinyume na maadili ya kazi yake?”

Wanachojua TFDA

Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Mashariki, Emmanuel Nkilingi anakiri kuwa wamewahi kupokea taarifa zinazohusiana na ghala hilo, lakini hawajazifuatilia. “Kazi ipo,” alisema meneja huyo huku akionyesha mshangao wa taarifa hizo.

“Kwa sababu najaribu kufikiria moja godauni (ghala) hilo ni la nani na tunawezaje kufika kukagua sababu hatushindwi na tutakachokikuta ni kitu gani?…na najaribu kujiuliza unaposema ana leseni ya taka rejea, nani anatoa leseni ya taka rejea na baada ya hapo inapelekwa wapi,” alisema Nkilingi.

Kesho, usikose simulizi ya namna bidhaa hizo zinavyofikishwa dampo na jinsi ushushaji unavyosimamiwa



Chanzo: mwananchi.co.tz