Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prof Mchembe akanusha hospitali nchini kujaa wagonjwa wa corona

6924f8348a9fc1694acff15cb1dd7ac5 Prof Mchembe akanusha hospitali nchini kujaa wagonjwa wa corona

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof Mabula Mchembe ameweka wazi kuwa, sio kweli Hospitali zimejaa wagonjwa wa corona kama inavyopotoshwa na baadhi ya watu wenye nia mbaya katika mitandao ya kijamii.

Prof Mchembe amesema hayo leo wakati alipofanya ziara katika hospitali binafsi za Agakhan na Kairuki ili kukagua hali ya utoaji huduma kwa wananchi na kuongea na viongozi wa hospitali hizo lengo ikiwa ni sehemu ya maboresho ya utoaji huduma katika Sekta ya Afya hapa nchini.

"Sio kweli kwamba hospitali hizi zimejaa wagonjwa wa corona kama inavyosemekana kwenye mitandao ya kijamii, hospitali zina uwezo wa vitanda zaidi ya 150 lakini sio vyote vina wagonjwa na wapo wagonjwa wa kila aina wanaohitaji huduma", amesema Prof Mchembe.

Mchembe ameupongeza ushirikiano uliopo kati ya hospitali binafsi, mashirika na zile za Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi wenye hali zote katika jamii.

"Nashukuru pia ushirikiano uliopo kati ya Hospitali binafsi na za mashirika binafsi kwa jinsi ambavyo zinashirikiana na Serikali, kikubwa ni kuwahudumia vyema wenzetu kama kawaida", amesema Prof Mchembe.

Aidha, Prof Mchembe ametoa onyo kwa hospitali zinazopandisha gharama za matibabu nchini bila kufuata taratibu na miongozo ya Serikali, huku akisisitiza kwamba, kuwa na tatizo la kupumua katika mfumo wa hewa sio kuumwa Corona.

"Niziase pia Hospitali, zisitumie nafasi hii, mtu kuwa na tatizo la kupumua kwenye mfumo wa hewa sio kwamba ana Corona, mbona mwanzo walivyokuwa wanawahudumia kabla ya haya yote haikuwa na gharama hizi, niwaase kwamba twende kwenye gharama ambazo zimewekwa na Serikali", alisisitiza Prof Mchembe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya Agakhan Dk Ahmed Jusabani ameweka wazi kuwa sio kweli Hospitali ya Agakhan imejaa wagonjwa wa Corona, huku akisisitiza kuwa wagonjwa wapo wa kila aina wakiwemo wagonjwa wa Saratani, mama wajawazito, magonjwa ya sukari na presha.

Aliendelea kusisitiza kuwa, wananchi wasikimbie huduma katika hospitali hiyo endapo watahitaji huduma, huku akisisitiza kutowachelewesha wagonjwa wanaohitaji huduma ili kuleta tija ya tiba zitazotolewa katika hospitali hiyo.

Naye, Mkurugenzi wa Hopitali ya Kumbukumbu ya Kairuki, Dk Asser Mchomvu amewatoa hofu wananchi juu ya tangazo la gharama za juu za matibabu hasa kwa wenye shida za mfumo wa upumuaji katika hospitali hiyo na kusisitiza kuwa tangazo hilo sio halali na hawalifahamu kwani halina muhuri wala saini ya Mkurugenzi wa hospitali hiyo.

"Zaidi ya asilimia 80 ya wateja wetu ni wa mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa, nataka kuwaondolea hofu wananchi hususan wateja wetu kwamba, lile tangazo ambalo lilitoka kwenye mitandao ya kijamii, sio kweli na hata sisi tulishangaa, na lingekuwa la kwetu, lingekuwa na muhuli wa Hospitali na lingekuwa na saini yangu ili liweze kutambulika", amesema Dk Asser Mchomvu.

Chanzo: habarileo.co.tz