Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pombe ni hatari kabla na baada ya Chanjo ya COVID-19

Da225a979a2d31eeab84ef503a5f8891 Marufuku kutumia pombe kabla na baada ya kuchoma chanjo

Thu, 5 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wataalamu wa afya wameeleza mambo ya kuzingatiwa kabla na baada ya kupata chanjo ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa covid-19, ikiwamo kutokunywa pombe kabla na baada ya kupata chanjo hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Afya kwa Umma wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Ama Kasangala amesema pia ni muhimu kama mtu ana maradhi apate tiba kwanza apone kabla ya kupata chanjo hiyo.

"Chanjo ni muhimu ila ukifika katika kituo cha kutolea huduma za afya utatoa historia ya hali yako watu wazingatie hili, kama una magonjwa upo katika matibabu ya magonjwa ambayo sio ya kudumu ni vyema ukasubiri kwanza kupona ndipo utumie chanjo," alisema.

Dk Kasangala alisema hakuna tafiti zinazoonesha kuwa mtu akinywa pombe inaweza kuathiri ufanisi wa chanjo, hata hivyo inashauriwa kutotumia kabla na muda mfupi baada ya kupata chanjo.

Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Tafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Paul Kazyoba alisema kama mtu ana maradhi yanayomsumbua ikiwamo malaria, tumbo au kichwa na anaendelea na matibabu ya aina yoyote ni vyema akamaliza matibabu kwanza.

"Kwa sababu ukichanjwa kama kutatokea mabadiliko yoyote ndani ya muda mfupi uweze kujua kama yanatokana na chanjo au ugonjwa mwingine ulionao, mtu mwenye maradhi ya kudumu kama ukimwi atapewa maelekezo na wataalamu wa afya.”

"Ukipata chanjo unaendelea na maisha yako kama kawaida kama unafanya biashara endelea nazo kama ni kazi endelea nayo huku ukiangalia kama kuna mabadiliko yoyote na unahitaji msaada” alisema.

Kazyoba alisema chanjo husisimua mwili hivyo anayechanjwa anaweza kupata maudhi madogo madogo ikiwemo homa ya kiasi au kali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Mariam Amour alisema katika hali ya kawaida unywaji pombe kupita kiasi huwa unashusha kinga.

"Sasa basi wakati unapata chanjo ni vema mwili wako uwe na kinga nzuri ili hiyo chanjo iweze kufanya kazi," alisema.

Alisema mtu anapopata chanjo anapaswa kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya kama kuvaa barakoa, kuepuka misukamano na kuosha mikono kwa maji tiririka.

"Pia chanjo inatumia wastani wa wiki mbili kuanza kufanya kazi, hivyo pia wazingatie mlo kamili,” alisema Dk Amour.

Kwa mujibu wa Dk Kasangala, miongoni mwa wasiotakiwa kupata chanjo ni wanawake wajawazito na akina mama wanaonyonyesha.

Wananchi jana waliendelea kujitokeza kwa wingi kupata chanjo kwenye mikoa mbalimbali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz