Kampuni ya dawa ya Marekani ya Pfizer imetia saini mkataba wa kuruhusu kidonge chake cha majaribio cha tiba ya Covid-19 kutengenezwa na kuuzwa katika mataifa 95 yanayoendelea.
Lakini haijumuishi nchi kadhaa ambazo zimekuwa na milipuko mikubwa ya Covid-19, ikiwemo Brazil.
Pfizer anasema kidonge hicho kinapunguza hatari ya ugonjwa mbaya kwa watu wazima walio hatarini.
Katika taarifa yake siku ya Jumanne, Pfizer ilisema makubaliano hayo yataruhusu watengenezaji wa dawa za kienyeji kuzalisha kidonge hicho "kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wake kwa urahisi duniani".
Pfizer haitapokea mirabaha ya mauzo katika nchi zenye mapato ya chini na ilisema itaondoa mirahaba katika mataifa yote yaliyojumuishwa katika makubaliano hayo huku Covid ikisalia kuwa dharura ya afya ya umma iliyotambuliwa na Shirika la Afya Duniani.
Mapema Novemba, Pfizer alisema majaribio ya kimatibabu yanaonyesha kuwa kidonge chake cha Covid-19, Paxlovid, kinapunguza kwa 89% hatari ya kulazwa hospitalini au kifo kwa wagonjwa wazima walio katika hatari kubwa.