Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacha wawili walioungana kutenganishwa Muhimbili

5c90081c86faf334fbd07c754a3edbb8 Pacha wawili walioungana kutenganishwa Muhimbili

Wed, 29 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ya jijini Dar es Salaam inatarajiwa kufanya upasuaji mkubwa Julai 1,2022 wa kutenganisha watoto pacha wawili wenye umri wa miezi tisa, waliozaliwa wakiwa wameungana sehemu ya kifua, tumbo na ndani wameungana ini, huku kila mtoto akiwa na ini lake.

Upasuaji huo unaotarajiwa kuchukua saa sita hadi saba utaifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu Afrika kufanya upasuaji huu, baada ya Afrika Kusini na Misri.

Daktari Bingwa Mshauri Mwelekezi Upasuaji wa Watoto,Dk. Petronila Ngiloi, amesema watoto hao walizaliwa Septemba 21,2021 kwa njia ya upasuaji wakiwa na kilo 4.9, wote kwa pamoja katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu.

" Walipewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando na baadaye kuletwa Hospitali ya Taifa Muhimbili tarehe 12 Novemba 2021, wakiwa na kilo saba ambapo sasa wana kilo 13.3. Ni wakazi wa Kijiji cha Mwabayande, Kata ya Mwigwa,” amesema,

Dk Ngiloi ameeleza kuwa kufanyika kwa upasuaji huu kunatokana na usimamizi mahiri wa menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili wa kuimarisha miundombinu stahiki ya kutolea huduma hizo, ikiwemo vyumba vya upasuaji na ICU zenye vifaa vya kisasa kuhimili aina hiyo ya upasuaji, pamoja na kusomesha watalamu wa kutoa huduma hizo kwa kiwango cha ubobezi.

Amesema upasuaji huo ni mkubwa, hivyo watoto hao wasingeweza kutenganishwa wakiwa na umri mdogo na uzito mdogo, kwa sababu wanapokuwa wakubwa kuanzia miezi saba hadi kumi matokeo ya upasuaji ni ya usalama zaidi, kwani wanaweza kuhimili hata dawa za usingizi na ganzi kulingana na aina ya upasuaji watakaofanyiwa.

"Kama wangepelekwa nje ya nchi, upasuaji huu ungegharimu karibu Sh milioni 120 ikijumuisha gharama za usafiri wa mama, watoto wawili na msindikizaji mmoja, pia kuna gharama za ziada za kufanya maandalizi ya watoto hawa ikiwemo lishe, na matibabu mengine ili kufikia kiwango cha kufanyiwa upasuaji wa kutenganishwa,"amebainisha.

Upasuaji kama huo ni mara ya tatu kufanyika hapa nchini ambapo mara ya kwanza ulifanyika mwaka 1994, ukihusisha watoto wawili wa kiume waliokuwa wameungana kwenye tumbo.

Upasuaji wa pili ulifanyika mwaka 2018 ukihusisha watoto wawili wa kiume wanaoishi Kisarawe, ambao wana miaka mitatu na miezi tisa sasa na wanaendelea vizuri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live