Dar es Salaam. Jopo la madaktari nchini Saudi Arabia, limejiridhisha pacha walioungana Maryness na Anisia Benatus wanaweza kutenganishwa bila kuwepo na kikwazo chochote.
Majibu hayo yametolewa ikiwa ni muda kupita tangu pacha hao wawasili nchini humo Julai 8, 2018 wakitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Akizungumza leo Agosti 27, 2018 na Mwananchi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma MNH, Aminiel Aligaesha amesema baada ya kufika Saudi Arabia madaktari hao walianza kuchukua vipimo upya.
“Waliwafanyia tena vipimo upya na wameweza kujiridhisha kwamba upasuaji wa kutenganishwa kwa pacha hao utawezekana hivyo kwa sasa wanawaandaa na wanatarajia kuwatenganisha miezi mitatu ijayo,” amesema Aligaesha.
Hii ina maana kwamba upasuaji huo huenda utafanyika Desemba.
Pacha hao wa kike waliozaliwa katika kituo cha Afya Misenyi mkoani Kagera Januari mwaka huu, wameungana kifuani hadi miguuni.
Anisia na Maryness Julai mwaka huu waliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mfalme Khalid mjini Riyadh wakiandamana na mama yao na kundi la madaktari.
Pacha hao watafanyiwa upasuaji baada ya Mfalme Salman kutoa idhini ya kufanyika kwa upasuaji huo kwa gharama ya Serikali ya Saudia.
Pacha wa Muhimbili
Katika hatua nyingine Aligaesha amewazungumzia pacha walioungana ambao walizaliwa Vigwaza mkoani Pwani kuwa wanaendelea vizuri chini ya uangalizi wa madaktari Muhimbili.
Amesema madaktari wanaendelea na maandalizi baada ya kujiridhisha kwamba wanaweza kuwafanyia upasuaji wa kuwatenganisha.
“Tunategemea kuwa miezi miwili ijayo hawa nao watatenganishwa,” amesema Aligaesha.
Pacha hao walizaliwa Julai 12 kwa njia ya kawaida eneo la Vigwaza wakati mama yao akiwa njiani kuelekea hospitali.