Hospitali ya Taifa ya Muhimbili leo inatarajia kuwafanyia upasuaji wa kuwatenganisha pacha walioungana kifuani.
Upasuaji huo unakadiriwa kutumia saa saba na utafanywa na wataalamu wa afya 31 kutoka Tanzania na Ireland ambao wanatokea Shirika la Operation Child Life.
Tanzania itakuwa nchi ya tatu baada ya Misri na Afrika Kusini katika bara la Afrika kufanya upasuaji mgumu zaidi kwa pacha walioungana.
Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa magonjwa ya watoto kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Petronila Ngiloi alisema hospitali imefanya maandalizi ya kutosha kwa kuwa mwanzoni mwa mwezi huu walianza na upasuaji wa kwanza wa kupandikiza nyama.
Dk Ngiloi alisema pacha hao wameungana kifuani na kuna sehemu kubwa ya uwazi kwenye kitovu wanachotumia pamoja. “Muunganiko wa viungo vya ndani ni sehemu kubwa ya ini imeungana, ingawa kila mmoja analo lake, kulinganisha na pasuaji mbili tulizofanya awali, hii ni ngumu zaidi kwa kuwa kuna muunganiko mkubwa wa ini, ndani pia kuna uwazi mkubwa kwenye kitovu wanachotumia pamoja. Tuna hakika upasuaji huu utakuwa salama na tutafanikiwa,” alisema.
Serikali ingelazimika kutumia hadi Sh120 milioni endapo pacha hao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu, lakini kwa kuwa upasuaji huu unafanyika nchini inakadiriwa kutumia hadi Sh50 milioni.
ADVERTISEMENT Jopo la upasuaji limejumuisha jopo la madaktari bingwa wa upasuaji watoto, upasuaji viungo watoto, upasuaji ini, wataalamu wa dawa za usingizi, wataalamu wa uangalizi maalumu, wataalamu wa radiolojia, wauguzi na wataalamu wa maabara. Wataalamu kutoka nje ni watano, wakiongozwa na Profesa Martin Corbally.
Naye Daktari Bingwa Upasuaji wa Watoto, Zaitun Bokhary alisema watoto hao wanachangia mshipa mmoja wa damu unaotoa damu kwenye ini kupeleka kwenye moyo.
Alisema watoto hao walizaliwa kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa na kuletwa Muhimbili Novemba mwaka jana, wakiwa na uzito wa kilo saba na sasa wana uzito wa kilo 13.3.
“Uongozi wa Hospitali ya Muhimbili chini ya Mkurugenzi Mtendaji Profesa Lawrence Museru amesaidia kuimarisha miundombinu ya hospitali, kuwezesha uwepo wa vifaa vya kisasa, wafanyakazi wenye ujuzi na uwepo wa vyumba vya wagonjwa mahututi vya kutosha. Hii itafanikisha upasuaji huu kuwa na mafanikio makubwa,’’ alisema Bhokary.
Alisema kuwa imechukua muda kufanya upasuaji huo kwa sababu kwa kawaida inabidi watoto wafikie kati ya miezi saba hadi 10 ili kuhakikisha matokeo ya upasuaji ni salama zaidi.
Alisema umri huo unashauriwa kitaalamu kwa kuwa wanaweza kuhimili dawa za usingizi na ganzi kulingana na aina ya upasuaji watakaofanyiwa.
Baada ya upasuaji huo wataalamu hao watajigawa katika timu mbili ambazo zote zitakuwa na wataalamu sawa.
Alisema timu hizi zitagawana majukumu kwa kila mtoto ili kutengeneza nafasi zaidi ya kila mtoto kuhudumiwa kwa usawa na muda wa kutosha. Watoto hao wanatarajiwa kuwa hospitalini hapo kwa muda wa mwezi mmoja baada ya upasuaji kwa matibabu zaidi.
Esther Simone, mama wa watoto pacha waliotenganishwa mwaka 2018 kutoka Kisarawe, alisema watoto wake wanaendelea vizuri hivi sasa baada ya kutenganishwa na mwanzoni hakutegemea wangetenganishwa salama.