Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacha waliotenganishwa waanza maisha mapya

26373 PACHA+PIC TanzaniaWeb

Sat, 10 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watoto pacha waliokuwa wameungana na kutenganishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana walianza maisha mapya wakiwa nyumbani baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali.

Mapacha hao, Gracious na Precious Mkono na wazazi wao wamerejea nyumbani Kimara-Kigogo wilayani Kisarawe baada ya kukaa hospitali kwa miezi minne.

Wiki mbili zilizopita pacha hao waliruhusiwa kurejea nyumbani, lakini ilishindikana baada ya uchunguzi uliofanywa na MNH kubaini uwepo wa mazingira duni ya nyumba yao.

Watoto hao walifanyiwa upasuaji wa kihistoria kuwatenganisha Septemba 23 katika hospitali hiyo baada ya kuzaliwa wakiwa wameungana kifuani na tumboni.

Upasuaji wa watoto hao uliofanywa chini ya madaktari bingwa tisa wa Tanzania kwa ushirikiano na bingwa wa upasuaji wa maini kutoka Ireland, unaongeza rekodi ya Muhimbili ambayo kwa mara ya kwanza ilifanya hivyo 1994.

Akizungumza akiwa na uso wenye tabasamu, mama wa watoto hao, Esther Mkono aliliambia Mwananchi kuwa ana furaha ya aina yake kurejea nyumbani akiwa na watoto wake wakiwa salama.

Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto wa MNH, Petronila Ngiloi alisema walitarajia kuwaruhusu mapema, lakini tatizo lilikuwa hali halisi ya familia hiyo kuwa duni, hivyo watoto hao wangeshindwa kuimudu.

Novemba 7, Benki ya UBA ilijitolea kuwajengea nyumba watoto hao na kuwapatia bima za afya za miaka 10 pamoja na fedha taslimu Sh2 milioni ambazo zilichangwa na wafanyakazi wao.

Akiwazungumzia watoto hao, Ofisa Ustawi wa Jamii wa MNH, Emmanuel Mwasota alisema mara baada ya kuzaliwa sehemu ya jamii wanayotoka ilihisi ni mkosi, dhana ambayo si sahihi, hivyo msaada huo utasaidia kuitokomeza.

Baba wa watoto hao, Michael Mkono alipopewa nafasi ya kuzungumza msaada huo aliishia kusema, “wababa hoyeee.”

Chanzo: mwananchi.co.tz