Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacha waliotenganishwa kutoka hospitali wiki ijayo

Sat, 20 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema wiki ijayo itawaruhusu pacha waliotenganishwa baada ya baadhi ya taratibu kukamilika, ikiwa ni pamoja na sehemu bora watakayoishi.

Pacha hao Gracious Nyamiri (Kulwa) na Precious Telya (Doto) walifanyiwa upasuaji wa kihistoria wa kuwatenganisha Septemba 23, 2018 katika hospitali hiyo baada ya kuzaliwa wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo.

Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo leo Ijumaa Oktoba 19, 2018 mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa Umma wa MNH, Aminieli Aligaesha amesema pacha hao hawakuruhusiwa kurejea nyumbani kutokana na mazingira waliyokuwepo katika nyumba watakayokwenda kuishi.

“Watoto hawa wanaendelea vizuri hatuwezi kuwaruhusu kimya lazima umma ujue na wiki ijayo tutawaruhusu. Kuna mambo mengine mengi ambayo jamii itafahamishwa,” amesema Aminieli.

Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto MNH, Petronila Ngiloi amesema  walitarajia kuwaruhusu mapema lakini tatizo ni maisha halisi ya familia hiyo,  watoto hao watashindwa kumudu.

Amesema Muhimbili ina malengo ya kuwafuatilia pacha hao, “kuwaruhusu sawa ila tungependa sana kujua mazingira ambayo wanaenda, bibi wa watoto amesema wanaishi kijijini na mazingira si mazuri sana.”

“Tukiangalia katika historia si kwamba tunawapa kipaumbele ila ni watoto wanaotengeneza historia yetu, tunahitaji kuwafuatilia.”

Bibi wa pacha hao, Aksa Mbega amesema hospitali ilitoa majina ya mwanzo na familia ikawapatia majina ya pili, “Nyamiri na Telya ni majina ya kikoo ya kabila letu la Kimasai, hatuwezi kusema maana halisi ya majina haya sababu ni ya babu zetu wa zamani.”

Chanzo: mwananchi.co.tz