Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ORCI: Kutopokea majibu ya Saratani ni hatari kwa taifa

Saratani Pic Ofisa Habari wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Masoud kassanga akitoa elimu ya ugonjwa wa Saratani

Sat, 8 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Mkurugenzi wa Kinga wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk Crisprin Kahesa amesema, Watanzania wengi wanaogopa na hawapo tayari kupokea majibu ya vipimo vya saratani jambo ambalo ni hatari kwa taifa.

Changamoto hiyo inakuja wakati ambapo takwimu za taasisi hiyo inaonyesha, asilimia 75 ya wanawake wanaofika katika taasisi hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi wanakutwa na ugonjwa huo katika hatua za mwisho.

Kufuatia hali hiyo, ORCI imetangaza huduma za uchunguzi wa saratani bure katika maonyesho ya Kimataifa ya 47 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF).

Akizungumza leo Julai 8 2023 na Mwananchi digital Mkurugenzi wa Kinga wa Ocean Road, Kahesa ambaye ni daktari bingwa wa saratani amesema mbali na uchunguzi wanatoa elimu kuhusu dalili, matibabu na namna ya kuepuka saratani.

Amesema matumizi ya vyakula vya viwandani, unene kupita kiasi na matumizi ya tumbaku vina mchango mkubwa la ongezeko la wagonjwa wa saratani.

Amesema ni muhimu jamii kutambua kuwa uchunguzi na tiba za awali ndio usalama kwa wagonjwa na taasisi hiyo imejipanga kutoa huduma ndani na nje ya nchi na kupanua wigo wa huduma za tiba za utalii kwa kutumi mashine za kisasa.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda la ORCI, Naomi Japhet ameiomba taasisi hiyo kuanzisha kampeni ya kuzunguka kwenye jamii kutoa elimu zaidi ya ugonjwa wa saratani.

Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliwahi kunukuliwa akisema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaweka mzigo mkubwa kwenye sekta ya afya na kwamba japo wana mipango mizuri ya kukabiliana na saratani lakini changamoto imekuwa ni fedha.

Waziri ummy aliyasema hayo w akizindua taarifa ya Taasisi ya Lancert Oncology iliyokuwa ikielezea hali ya ugonjwa huo nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa upande wa Afrika Mashariki.

Amesema, ugonjwa wa saratani umeua watu 25,000 mwaka 2020 na kuufanya ugonjwa huo kuwa tishio zaidi ya Uviko-19 ilioua watu chini ya 1,000 hapa nchini Mwananchi. Fikiri Tofauti.

Chanzo: Mwananchi