Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyumba kwa nyumba ugawaji vyandarua vyenye dawa

NET Nyumba kwa nyumba ugawaji vyandarua vyenye dawa

Sat, 29 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMPENI ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu kwa kaya bila malipo imeingia katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Singida na ili ifanikiwe serikali kupitia mawakala wake inapita nyumba kwa nyumba mijini na vijijini kuwaandikisha walengwa watakaonufaika na mpango huo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Rashid Maftaa alisema mpango huo ni muendelezo wa mikakati ya serikali ya kutokomeza ugonjwa huo na akawataka wananchi wote katika kila kaya kuandikishwa.

Kwa kupitia mpango huo alisema kila watu wawili watakaoandikishwa watapewa chandarua kimoja chenye ukubwa wa futi tano kwa sita bure.

“Kwa hiyo tunataka watu wote katika kila kaya waandikishwe ili wanufaike na mpango huu. Tukimaliza mikoa ya Iringa, Dodoma na Singida, tutaelekea katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Tanga," alisema.

Kwa mkoa wa Iringa wenye wakazi zaidi ya milioni 1.2; Maftaa alisema tayari vyandarua zaidi ya 675,000 vimetengwa kwa watu wawili wawili walioandikishwa na utaratibu wa usambazaji wake umeanza jana, Ijumaa.

Akizungumzia mafanikio ya mpango wa ugawaji wa vyandarua nchini kote katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Naibu Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Malaria nchini, Dk Samwel Nhiga alisema lengo lilikuwa kugawa vyandarua milioni 23, lakini vilivyogaiwa ni zaidi ya milioni 47 na hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 100.

Dk Nhiga alisema vyandarua hivyo vimekuwa vikitolewa kupitia programu mbalimbali za serikali na kuwafikia walengwa wake kwa kupitia kaya zao, shule za msingi na kliniki ya mama na mtoto.

Alisema serikali ya awamu ya tano imetumia zaidi ya Sh bilioni 8.3 kwa ajili ya kutokomeza malaria nchini katika kipindi chake chote na kwamba gharama hiyo inatarajia kuongezeka kwa kadri mahitaji yatakavyoongezeka.

Alitoa mwito kwa walengwa kuvitumia vyandarua hivyo vinavyosambazwa na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) kwa lengo lililokusudiwa ili kuwezesha mipango ya serikali kufikiwa ndani ya muda uliopangwa.

Chanzo: habarileo.co.tz