Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyota ya Dk Mwele yazidi kung’aa

21248 Mwelel+pic TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Espen), wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Mwele Malecela ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa WHO anayeshughulikia magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTD).

Dk Mwele ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo wa Afrika Aprili mwaka jana, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) kabla ya kuvuliwa wadhifa huo na Rais John Magufuli Desemba 16, mwaka 2016.

Taarifa ya uteuzi wake mpya iliwekwa katika akaunti ya Twitter ya Shirika hilo ikieleza kuwa uteuzi huo ulifanyiwa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom.

Tangu kuteuliwa kwake, Dk Mwele aliongoza mradi wa Espen ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2016 hadi 2020 ukiwa na lengo la kukabiliana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwa kutoa vifaa tiba, elimu na dawa.

Magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni pamoja na matende, mabusha, kichocho, minyoo ya tumbo na usubi.

Kwa uteuzi huu, Dk Mwele ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, atahusika kusimamia miradi ya kupunguza magonjwa ya Kitropiki yasiyopewa kipaumbele ambayo yapo katika nchi 149 duniani.

Chanzo: mwananchi.co.tz