Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyama inayokatwa kwenye gogo hatari kwa afya

24957 Nyama+pic TanzaniaWeb

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) imewatahadharisha Watanzania kuhusu matumizi ya nyama inayouzwa kwenye mabucha yasiyotumia misumeno na mashine katika ukataji na badala yake kutumia shoka kwa kuegesha kwenye magogo.

TMB imesema nyama inayokatwa kwenye magogo si salama inaweza kumletea madhara ya kiafya mlaji kwa kuwa magogo hayo yanahifadhi vimelea vya maradhi.

Ofisa wa nyama wa bodi hiyo, Edgar Mamboi akizungumza na waandishi wa habari jana alisema vimelea hivyo hutokea kwa kuwa gogo halisafishiki vyema hivyo vijidudu kuendelea kubaki.

“Hakuna namna yoyote ambayo gogo linaweza kusafishwa na kuondoa uchafu wa kutwa nzima, hapo ndipo vijidudu vinapopata nafasi na nyama inapowekwa vinahamia huko, ndio sababu tunasema ni hatari kwa afya,” alisema.

Alisema vipande vidogo vya gogo vinavyotoka wakati shoka linapogonga mfupa, huingia kwenye nyama na kuiondoa kwenye usalama.

Kufuatia hilo bodi hiyo imesisitiza Watanzania kuacha kununua nyama kwenye bucha ambazo bado zinatumia mfumo huo wa kizamani na kuhamia kwenye zile zinazokata kitoweo hicho kwa mashine.

Mamboi alisema kwa muda mrefu, TMB imekuwa ikiwaelimisha na kuwaagiza wenye bucha kutumia mashine lakini bado wapo wanaokiuka agizo hilo.

Alisema wamekuwa wakiendesha msako ili kubaini wanaotumia magogo na hatua kuchukuliwa ikiwamo kufungiwa.

Kaimu msajili wa bodi hiyo, Imani Sichalwe alisema hiyo ni hatua mojawapo ya kuhakikisha Watanzania wanakula nyama kama inavyoelekezwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO).

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo na kuzalisha nyama nyingi, wastani wa ulaji wa nyama ni kilo 15 kwa mwaka wakati FAO inaelekeza kilo 50. TBM imebaini kuwa moja ya sababu ni gharama za kitoweo hicho.

Pamoja na mashine za kukatia, bodi hiyo imeweka nguvu katika kuhamasisha matumizi ya mizani ya dijitali ili kuwawezesha wateja kununua nyama kulingana na viwango vya fedha walizonazo.

“Kwenye mabucha ya kawaida bei ya nyama inaanzia Sh5,000 sasa kwa mwenye kipato kidogo anaweza kushindwa kumudu ndio sababu tunataka itumike mizani ya dijitali ili sasa nyama ipimwe kulingana na fedha aliyonayo,” alisema Sichalwe.

Ni muhimu kwa binadamu kula nyama kwani ina umuhimu mkubwa mwilini kutokana na viini lishe vya kipekee ambavyo kitoweo hicho ambavyo havipatikani kwenye mboga nyingine.”

Sichale alisema nyama salama inaanzia kwenye ufugaji ambapo mfugaji anatakiwa kufuata kanuni na taratibu za ufugaji, kusafirisha mifugo kwa kuzingatia viwango na kuchinjwa katika machinjio zilizokidhi vigezo.

Kuhusu madai nyama nyekundu ina madhara alisema hutokea endapo itakuwa kwa kiwango kikubwa na itakuwa haijahifadhiwa katika mazingira salama.

“Nyama bora ni ile inayotokana na mifugo iliyotunzwa kwa kuzingatia viwango vya uzalishaji bora. Pia, nyama inatakiwa iuzwe kwenye mabucha yaliyokidhi vigezo, usile nyama ya mezani au inayotembezwa mtaani,”.

Chanzo: mwananchi.co.tz