Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Njia salama ya kufunga uzazi ni hii hapa….

Kujifungua Kwa Njia Ya Upasuaji.png Njia salama ya kufunga uzazi

Sun, 19 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Matibabu ya kufunga kizazi kwa njia ya upasuaji wa matundu madogo ‘laparascopy’ yameanza kutolewa nchini. Teknolojia hiyo mpya inawawezesha madaktari kufanya upasuaji bila kuchana tumbo na kisha kufungua iwapo mama atahitaji kupata mtoto mwingine siku za baadaye. Uwepo wa teknolojia hiyo umeelezewa utawawezesha wanandoa waliotosheka na watoto kufanya uamuzi wa mama kufunga kizazi kwa njia salama itakayomwezesha kufanya uamuzi mwingine iwapo atabadili mawazo.

Asilimia 99 ya wanawake nchini walioamua kufunga kizazi walipewa huduma hiyo kwa njia ya upasuaji mkubwa ambao hata hivyo kwa mujibu wa wataalamu wa afya hauruhusu mwanamke kupata tena ujauzito. Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na mbobezi wa tiba ya upasuaji wa matundu kwa kinamama kutoka Hospitali ya CCBRT iliyoko jijini Dar es Salaam, Daniel Michael alisema mpaka sasa wamefanya upasuaji wa kufunga kizazi kwa wanawake wanne tangu kuanza kwa huduma hiyo mapema mwaka huu. “CCBRT tumeona ni faraja tunampatia mgonjwa wetu nafasi ya kuamua njia gani atumie, kupitia teknolojia hii tunaweza kufunga kizazi, lakini pia ataweza kufunguliwa. “Kupitia hii mashine ukilinganisha na ule upasuaji wa zamani, ukifunga umefunga jumla, lakini hii tunafungua na kuunganisha tena mirija,” alisema Dk Daniel aliyepata utaalamu wa ubobezi wa upasuaji huo nchini India alikowafanyia upasuaji wagonjwa zaidi ya 15 kwa mafanikio. Dk Daniel alisema awali kufunga kizazi ilikuwa ni moja ya njia ya uzazi wa mpango ambao haurudi nyuma, kwani mama akiamua kufunga kizazi anakua ameshamaliza kuhusu watoto. “Kuna upasuaji wa kufunga kizazi, mama anachanwa tumbo kwa ukubwa wa sentimita saba, hii tunafanya kizazi kikiwa juu baada ya mama kujifungua, lakini kwa sasa imekuja hii ya kufunga kizazi kwa njia ya matundu madogo ambayo ni salama zaidi,” alisema. Akieleza kwa kina, Dk Daniel alisema wakishaingia ndani wanaweza kuweka pete maalumu kwenye mrija na ikikaa pale, siku mama akitaka kuzaa tena wanamfanyia upasuaji mwingine wa matundu na kuitoa pete hiyo na mama kupata ujauzito. “Muda mwingine mtu anafunga kizazi, lakini wengine huwa wanajutia anasema natamani kupata mtoto mwingine, lakini tukimfunga kwa njia hii anaweza kupata nafasi nyingine ya kubeba ujauzito,” alisema. Hata hivyo, alisema kabla ya upasuaji, mama hupewa ushauri nasaha kwa kuambiwa faida na hasara zake kwa muktadha wa tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika.

Faida Dk Daniel alisema faida za upasuaji huo ni pamoja na mgonjwa kutopata makovu mwilini yanayosababishwa na kufungwa kizazi. “Mshono si mkubwa ukilinganisha na njia nyingine ile ya kuchana kabisa, kwa njia hii mgonjwa anaridhika kwa upasuaji rafiki hauharibu maumbile anabaki hana kovu. “Ni bora zaidi na pia anapona haraka baada ya upasuaji hadi anaruhusiwa ndani ya saa 12, pia haina maumivu makali sababu ni matundu kidogo,” alisema. Alitaja faida nyingine kuwa ni upasuaji huo hufanywa kwa dakika 35 pekee na ni teknolojia inayoweza kuipa uhai mirija kama mama atataka kupata mtoto baadaye ukilinganisha na upasuaji mkubwa ambao unachukua saa moja mpaka mbili. Pia alisema mgonjwa hapotezi damu nyingi wakati wa upasuaji, bali ni damu kidogo na anaruhusiwa baada ya saa chache kurudi nyumbani na baada ya saa nne anaruhusiwa kula chakula chochote.

Hasara Mbali na huduma hiyo kuwa na faida, Dk Daniel alizitaja changamoto zinazoweza kutokea wakati wa kufanya upasuaji huo iwapo umakini hautazingatiwa. “Hasara yake ni kama ikitokea changamoto yoyote itabidi upasuaji mkubwa ufanyike, hivyo inahitaji utaalamu wa hali ya juu kwa kuwa tunatumia mikasi, uzi unaweza kutoboa hata utumbo kama mtaalamu asipokuwa makini. Daktari inabidi awe na uhakika na anachokifanya,” alisema. Alisema kutokana na changamoto hizo, mgonjwa lazima aelezwe kwa kupewa ushauri kabla ya kufanyiwa matibabu hayo, ili ajue faida na hasara ikiwemo uwezekano wa mimba kutunga nje ya kizazi. “Akiona faida ni nyingi kwake kuliko hasara anafanya uamuzi.” Alisisitiza ikiwa kiasi cha nyama za mrija zilikatwa sana wakati wa zoezi la awali itakua vigumu kuunganisha tena mirija ya mayai. Alitaja changamoto kubwa ni gharama za huduma hiyo hasa kwa wagonjwa wanaolipia ikilinganishwa na wale wanaotumia bima. “Gharama za upasuaji huo kwa njia ya matundi ya kufunga uzazi ni Sh1 milioni na unapotaka kufungua gharama zake ni nyingine pia,” alisema. Dk Daniel alitaja huduma nyingine zinazotolewa na upasuaji wa aina hiyo kuwa ni kutoa kizazi, kuondoa mimba zilizotunga nje ya kizazi, kuondoa vimbe katika kizazi na matibabu kwa wagonjwa wa saratani ya kizazi.

Uzazi wa mpango Licha ya kufunga kizazi, njia mbalimbali ambazo wanawake wamekuwa wakizitumia kupanga uzazi zinadaiwa kuwa na matokeo hasi kwa baadhi yao. Daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya kinamama, Issa Rashid alisema njia hiyo ni nzuri, kwani haitamuacha mama na makovu. Alitaja faida za mwanamke kufunga uzazi kuwa ni kubaki na idadi ndogo ya watoto alioamua kuwa nao ambao ataweza kuwatunza, kuwajali na kuwafuatilia. “Kufunga kizazi ni afya kwa mwanamke, kwani inampa nafasi ya kufanya uamuzi na kutokuwa na hofu ya kushika mimba iwapo hana uhitaji kwa wakati huo na pia inampa muda wa kuwaangalia na kuwalea vizuri wale alionao,” alisema. Dk Issa alisema uzazi huchosha mwili wa mwanamke, “anapobeba mimba miezi tisa anakutana na changamoto nyingi za uzazi ikiwemo kuchanika wakati wa kujifungua, lakini kwa kuwa teknolojia inakua wataalamu wamekuja na mbinu nzuri zaidi na rafiki.” Mkunga mtaalamu, Agnes Ndunguru alisema njia hiyo ni nzuri kama uzazi wa mpango wa kudumu ambao huwa haurudi nyuma. “Wakunga huwa tunashauri kinamama waliopata watoto wengi kufanya uamuzi wa kufunga kizazi tukisisitiza kuwa lazima wawashirikishe wenza wao, lakini upasuaji huu ulioboreshwa ni mzuri zaidi mama akautumia baada ya kujiridhisha,” alisema Agnes.

Chanzo: Mwananchi