Utokaji wa damu ukeni kwa matone kwa mjamzito wa wiki 20 za mwanzo inachukuliwa kama mimba kutishia kutoka, kitabibu hujulikana kama Threatened abortion.
Kutokwa matone ya damu ukeni ni kitu kinachotokea kwa wajawazito wengi katika kipindi cha miezi ya awali ya ujauzito pasipo kusababisha tatizo lolote.
Kwa kawaida hali hii huambatana na maumivu chini ya tumbo huku pakiwa na damu ya kiasi tu. Pale daktari anapofanya uchunguzi wa kimwili atagundua mlango wa nyumba ya uzazi umefunga.
Vile vile pale mimba hii inapopimwa katika kipimo cha ultrasound huendelea kuonyesha uwepo wa kiumbe kilicho hai ingawa mimba inayotishia kutoka huweza kubadilika na kutoka yenyewe.
Sababu za kutokea tatizo hili huwa ni zile zile za mimba kuharibika ambazo haziko wazi ingawa yapo mambo ambayo yanahusishwa na tatizo hili.
Vihatarishi vya tatizo hili ni pamoja na kuwa na kichanga kisicho cha kawaida (mimba ikiwa chini ya miezi mitatu).
Matatizo ya chembe za urithi ni mojawapo ya chanzo cha kuwa na kichanga tumboni kilicho na hitilafu.
Kupata ajali au majeraha katika maeneo ya tumbo na kiunoni ni moja ya sababu ya tatizo hili.
Ikitokea katika miezi 4-6 yaani muhula wa pili wa ujauzito kwa kawaida inaweza kuhusishwa na matatizo kwa upande wa mama kuliko kwa mtoto, magonjwa sugu ikiwamo kisukari, shinikizo kali la damu, magonjwa ya figo na matatizo ya tezi inayotoa homoni za ukuaji wa mwili, kuwa na unene uliopitiliza na umri zaidi ya miaka 35.
Pia, upungufu wa homoni za kike, maambukizi ya virusi, dosari katika viungo vya uzazi ikiwamo udhaifu wa mlango wa uzazi, uwapo wa uvimbe, kondo la nyuma kuwa na hitilafu, mimba pacha na kuingiza vifaa vya kuoshea ukeni.
Mambo mengine ikiwamo dawa, matumizi ya vitu vyenye caffeine, pombe, tumbaku na dawa za kulevya.
Dalili kubwa ni kuona matone ya damu ukeni ingawa pia damu hiyo inaweza kuwa nyingi, hivyo ni vema kufahamu kuikadiria ilitoka kiasi gani na kwa kipindi gani. Pia kuangalia vitu vilivyomo ndani ya damu hiyo iwapo kuna vipande vya tishu ili kumweleza daktari wako atakayekutibu.
Maumivu ya chini ya tumbo yanaweza kuwa upande mmoja au pande mbili au katikati na kusambaa katika mgongo, makalio na katika sehemu za siri.
Matibabu ya tatizo hili itategemeana iwapo mimba hiyo haikutoka. Dawa ya Paracetamol ndio salama kwa maumivu haya ya kawaida, usitumie dawa kama Asprini na diclofenac.
Mgonjwa ataruhusiwa kurudi nyumbani na kupumzika endapo atachunguzwa na kubainika kuwa mlango wa nyumba ya uzazi umefunga, damu iliyotoka ilikua kidogo na haitoki tena, vipimo vya uchunguzi vitaonyesha kuwa hakuna tatizo.
Takwimu za shirikisho la madaktari wa magonjwa ya kina mama duniani zinaonyesha asilimia 50 ya wajawazito wanaopata tatizo hili wanafika muhula wa mwisho wa ujauzito na kujifungua salama.
Ili kuepukana na tatizo hilo kitabibu inashauriwa mjamzito aepuke unywaji pombe au vilevi, uvutaji sigara, utumiaji dawa kiholela na afike mapema katika huduma za afya anapopata dalili za magonjwa.