Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni muhimu sana wanaume kutokosa kliniki

04a9964c3367cfc2d0bba26247566e6d Ni muhimu sana wanaume kutokosa kliniki

Mon, 12 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“ WAPO wanaume wanaoona aibu kwamba nikienda na mke wangu kliniki watu wataniona nimeshikwa masikio (nimetawaliwa na mke)!” Anasema Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Iyunga jijini Mbeya, Dk Yusta Ndotela.

Tabibu huyo alikuwa anazungumzia ushiriki duni wa wanaume kwenye masuala ya afya ya uzazi ya wake zao jijini Mbeya.

Watalaamu wa tiba wanasema kwamba wanaume wengi wametawaliwa na dhana isiyo sahihi kwamba suala la mimba ni la mwanamke pekee kwa vile ndiye anayeibaba lakini wanasema ushiriki wa baba wa muda wote katika afya ya ujauzito aliyousababisha ni muhumu sana na yenye faida lukuki.

Kutokana na kutojua umuhimu wa ushiriki wao, wanaume wengi wamekuwa na visingizio lukuki alimradi wasiandamane na wake zao kliniki lakini wataalamu hao wanasema visingizio vinavyotolewa si vya msingi ikilinganishwa na faida zinazoweza kupatikana kwa uwepo wao kwenye huduma za afya tangu mimba inatungwa hadi mtoto kukua.

Akitoa mfano kuhusu ushiriki dunia wa wanaume, Dk Ndotela anasema takwimu za mwezi uliopita zinaonesha kwamba wanawake walioanza kliniki katika kituo chake wakiwa na ujauzito wa umri wa chini ya wiki 12 kama inavyoshauriwa, walikuwa 12.

Hata hivyo, waliokuja na wenzi wao walikuwa watatu tu. “Kwahiyo utaona mwamko bado ni mdogo sana. Mpaka sasa wajawazito wanaokuja na wenza wao kuanza kliniki ni chini ya wastani ya asilimia 25,” anasema.

Anasema wanaendelea kutoa elimu kwa wanaokuja kliniki wakishirikiana na watu wanaoitwa Mbata ambao wanatoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanaume kwenye huduma za afya za wenzi wao.

Faida za ushiriki wa wanaume Dk Ndotela anasema zipo faida nyingi za mwanaume kuongozana na mwenza wake kliniki wakati wa ujauzito. “Kwanza ni muhimu kutambua mwanamke anapopata ujauzito, jukumu la kutunza mtoto tangu angali tumboni ni la mke na mume na siyo jukumu la mmoja pekee.

Iwe kiafya, kisaikolojia mpaka atakapojifungua. Hali kadhalika jukumu la kuendelea kulea mtoto ni la wote pia,” anasema. Anasema mwanaume unapofika hospitali ukiwa na mwenzi wako, faida ya kwanza ni kutunza afya.

“Mnapofika, wote mtapata ushauri nasaha kisha mtapimwa hali za afya, Na hii siyo tu maambukizi ya VVU (virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi) bali yapo magonjwa mengine ambayo anaweza akayapata mama wakati wa ujauzito yakamdhuru mtoto tumboni au atakapojifungua akapata shida.

Magonjwa haya kama vile kaswende baba anapaswa pia kujua na kushirikiana na mwenza wake kuyatibu. “Mtapima wote wawili, mke na mume na kwa maana hiyo mkiwa katika hali salama mnajihakikishia kwamba mtoto atakuwa salama kwa sababu hata mama anapokuwa mjamzito mtakuwa bado mnakutana katika tendo la ndoa.”

Dk Ndotela anasema faida nyingine ya baba kumsindikiza mkewe kliniki ni pamoja na kujua kama ana matatizo yoyote yanayoweza kumhitajia kula aina fulani ya vyakula au kuhitaji kutofanya kazi (bed rest).

Anafafanua kwamba kwa kuwa mara nyingi wanaume ndio watoaji wa mkate, anaposikia kutoka kwa daktari kwamba mwenza wake anatakiwa kula vyakula vya aina fulani, inakuwa vyema zaidi kuliko anapokuja kuambiwa baadaye na mkewe.

Anaweza kudhani anajitungia kutokana na ulafi wake! “Tunapata kesi nyingi…. Mama amekuja kliniki anaambiwa anatakiwa kula aina fulani za vyakula. Anaporudi nyumbani na kumwambia mume wake, mume anamwambia unadeka.

Anampa maneno ambayo hayamtii moyo,” anasema. Kadhalika anafafanua kwamba mjamzito anapoonekana anahitaji mapumziko ya muda mrefu (bed rest), kama kauli haitatolewa na daktari mumewe akisikia mubashara, anaweza kudhani anataka kujidekeza.

“Kisaikolojia, mjamzito anaposindikizwa na mwenza anajisikia faraja kwamba waliutafuta ujauzito pamoja na wanapelekana hospitalini pamoja na kurudi nyumbani pamoja,” anasema.

Anasema mwanamke anapokuwa mjamzito anapata changamoto nyingi za kisaikolojia na hivyo ukaribu wa mwenza wake muda wote ni muhimu sana kwa faida ya mama na mtoto tumboni.

Anasema kufika kwa baba kliniki kunawezesha pia kusaidia katika kufanya maandalizi sahihi wakati wa kujifungua na baada kwani takwimu zinaonesha kuwa wanawake wengi wanaohudhuria kliniki peke yao maandalizi yao huwa duni ikilinganishwa na wanaoongozana na wenza wao.

Anatoa wito kwa wanaume kubadilika na kuwa na mtazamo chanya juu ya kushiriki katika mfululizo wa ufikaji na wenza wao kliniki kutokana na faida lukuki zinazopatikana.

“Wanaume watambue kuwa kuitwa mzazi wa mtoto kunaanzia tokea maandalizi ya kutungwa kwa mimba mpaka malezi baada ya mtoto kuzaliwa,” anasema.

Ushiriki wa wanaume wakiwa na wenza wao wajawazito wanaohudhuria katika kituo hicho cha Afya Iyunga hautofautiani na ule ulioanza kuonekana katika Kituo kipya cha Afya cha Nzovwe kilichoanza kufanya kazi hivi karibuni jijini Mbeya.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Leticia Mgeta anasema elimu inahitaji kwa wanaume kutambua umuhimu wa kushiriki kliniki na wenza wao.

Anasema akina baba wanaowasindikiza wenzi wao wajawazito kliniki ni wachache na anapotokea mmoja mmoja wanampongeza na kumtia moyo ili awe chachu ya kuhamasisha wanaume wengine.

Akitoa taswira halisi ya jiji la Mbeya juu ya ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya uzazi, Mganga mkuu wa jiji hilo, Dk Jonas Lulandala anasema bado ushiriki uko chini na kwamba hilo ni tatizo linalohitaji nguvu ya pamoja ya wadau kulishughulikia.

“Tatizo lipo lakini tumejaribu namna ya kuanza kulipunguza ili wanaume waweze kushiriki kwenye masuala ya huduma za uzazi. “Baba kama atashiriki kwenye suala zima la huduma ya uzazi, akifika pale kliniki atapata elimu.

Atajua ni lini wanaweze kuzaa yeye na mke wake, wazae watoto wangapi na waweke utofautishi wa mtoto mmoja hadi mwingine kwa muda gani,” anasema.

Mganga mkuu huyo anasema hali iliyopo ya umiliki wa uchumi kuwa chini ya wanaume katika familia nyingi linaleta pia msukumo wa umuhimu wa mwanaume kuambatana na mkewe kwenda kliniki.

“Hii itawezesha wanaposimamia upangaji bajeti za familia wazinga tie pia mahitaji ya msingi ya mama mjamzito,” anasema. Anaongeza: “Kama tunavyofahamu baba ndiye kiongozi wa familia, akiwa wa kwanza kulifahamu hili akashirikiana na mama itawezekana.

Lakini kama mama peke yake ndie atakuja kutoa elimu hii kwa baba, si akina baba wote watakubali kwa urahisi elimu anayoipata kwa mkewe. “Lakini kitu kingine tunafahamu mama akishakuwa mjamzito anahitaji mlo maalumu ili uweze kumjenga kiafya yeye na mtoto aliyembeba tumboni.

Suala hili litagusa uchumi. Sasa tukiangalia uchumi katika familia mara nyingi anayeudhibiti ni baba, hivyo kama baba atapata elimu palepale kliniki alikokwenda na mkewe ina maana haitohitaji nyumbani igeuke ajenda ijadiliwe tena.”

Anasema wanandoa kusindikizana kiliniki pia inaongeza upendo ndani ya nyumba. Dk Lulandala anasema wanachokifanya kwa sasa ni kuhamasisha akina baba kufika pamoja na akina mama hospitali ili wapate vipimo kwa pamoja, kupata elimu na pia mama anayekwenda na mwenza anapewa kipaumbele kuhudumiwa kwanza ili kuwapa morali zaidi wanaume waone hata wakienda hawakai muda mrefu.

Kusuasua huku kwa wanaume kwenye masuala ya afya ya wazazi kunaifanya Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuja na mkakati madhubuti katika kuongeza ushiriki wa wanaume.

Mkakati huo ni kuwatumia madiwani na wenyeviti wa mitaa kila mmoja kutoa elimu kwenye eneo analoliongoza. Dulmohamed Issa, Meya wa jiji la Mbeya nasema hapendelei kuona wanaume wanaendelea kuwaachia wanawake jukumu la masuala ya afya ya uzazi peke yao.

Anasisitiza kuwa ni wakati wa jinsi zote kushiriki ili kuwezesha kuwa na jamii yenye ustawi. “Ni suala ambalo lipo na hata mimi linanisikitisha kwa sababu mimi binafsi mke wangu amezaa watoto watano na siku zote nilikuwa ninakwenda naye hospitali, toka mwezi wa kwanza tu anapopata ujauzito mimi na yeye mguu kwa mguu tunakwenda hospitali.

“Nitoe wito kwa wanaume wenzangu kwamba jamani mtoto wa kwetu wote… Ule mzigo tukimwachia mama peke yake si sahihi. Wakati wa ujauzito ni wakati wa kuwa naye karibu, umwoneshe mapenzi. Lakini katika hili kwakuwa ninao madiwani wenzangu ambao wana wananchi kwenye kata zao nao nitawatupia mzigo kwenye vikao vyao wazungumze hili.”

“Wenyeviti wa mitaa wahamasishe. Kwa sababu siyo kwamba mama ukishampa ujamzito ndiyo basi umtelekeze hapana. Yule mtoto akizaliwa haitwi bin mama anaitwa bin baba.”

“Lakini pia ukiachana na nafasi yangu ya umeya, kwa upande wa pili nikiwa sehemu ya viongozi wa dini nawasihi pia viongozi wa dini zote kuhakikisha wanatumia nyumba zao za ibada kuielimisha jamii juu ya jambo hili. Lisiishie kusisitizwa na wanasiasa pekee,” anasistiza meya huyo ambaye pia ni shehe wa msikiti mkubwa wa Isanga jijini hapa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz