Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni hatua kwa hatua, mikakati dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza- Waziri

9692 Magonjwa+pic TZWeb

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea yenye changamoto kubwa ya maradhi yasiyoambukiza.

Lakini juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya nchini, zinaonyesha siku moja Watanzania watayaepuka maradhi hayo.

Mwandishi wa Mwananchi, Herrieth Makwetta, hivi karibuni alizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuhusu hali hiyo na hapa anaeeleza kwa kina hatua zilizofikiwa hadi sasa katika kutekeleza mikakati ya kisera ya kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza.

Swali: Tunapozungumzia maradhi yasiyoambukiza, Tanzania ipo katika nafasi gani?

Jibu: Mwaka 2010, Shirika la Afya Duniani (WHO) ilitoa taarifa kwamba maradhi haya yanachangia asilimia 47 ya wagonjwa na katika 100, wanaofariki dunia, 60 hufa kwa maradhi yasiyoambukiza.

Takwimu hizo zinaonyesha, endapo hatua mahususi hazitachukuliwa za kupambana na kudhibiti maradhi hayo ifikapo mwaka 2020, takwimu zitapanda kutoka asilimia 47 hadi 60 na kwenye vifo pia itapanda kutoka asilimia 60 hadi 73.

Hapa nchini tunapata picha ya hali ya maradhi yasiyoambukiza kupitia utafiti wa Wizara ya Afya uliofanywa katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Mara na Kilimanjaro miaka ya 1990.

Lakini naomba nisiende huko, kwa sasa tunatumia utafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) wa mwaka 2012 na ndiyo ambao tunautumia mpaka leo.

Utafiti huo ulifanywa kwa kushirikiana na WHO, Wizara ya Afya na wadau wa afya na ndiyo unatupatia muhtasari wa maradhi haya yasiyo ambukiza nchini.

Utafiti huu ulionyesha asilimia 15.9 ya Watanzania wanavuta sigara na hiki ndicho kichocheo kikuu cha maradhi yanayoambatana na yale ya mfumo wa hewa, asilimia 29 wanakunywa pombe, asilimia 26 ni wanene kupita kiasi, asilimia 26 wana lehemu nyingi mwilini, asilimia 33.8 wana mafuta mengi mwilini.

Pia, ulionyesha kuwa asilimia 9.1 wanaugua kisukari na asilimia 25.9 walionekana kuwa na shinikizo kubwa la damu.

Tafiti hizo za muda kidogo zinatosha kuiweka nchi katika hatari ya wengi kuugua maradhi haya.

Swali: Serikali ilianzisha kampeni ya kuhamasisha watu kufanya mazoezi ‘Afya yako, mtaji wako’ ili kupambana na maradhi yasiyoambukiza, kampeni hii imeleta matokeo yoyote chanya?

Jibu: Kampeni hii ilikuwa ni matokeo ya utafiti ule wa mwaka 2012 ambapo robo ya wananchi waliohojiwa walisema hawafanyi mazoezi wala kazi za kutumia nguvu. Nakiri kwamba hatukufanikiwa kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa kampeni ya kufanya mazoezi, lazima niwe mkweli.

Tulianza vizuri, mategemeo yetu katika kila halmashauri na mkoa wangeendelea na utekelezaji wa kamepi hiyo ambayo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliianzisha.

Kuna baadhi ya Halmashauri naona waliendelea na zoezi lile na kuna zingine zimesitisha.

Tumekutana tena na viongozi wa mikoa na kuzungumza nao kwa lengo la kuona kuwa ipo haja ya kuizundua upya kampeni hii , licha ya baadhi ya mikoa inaendelea kufanya mazoezi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Swali: Kuna sera au mwongozo wowote wa kupambana na maradhi yasiyoambukiza? Na ni kitu gani mnakitilia mkazo?

Jibu: Mwaka 2016 Serikali tulitengeneza na kuzindua mkakati wa taifa wa kupambana na maradhi yasiyoambukiza kwa miaka mitano.

Ule mkakati ndiyo umeonyesha maeneo mahususi ambayo tutayafanyia kazi.

Na eneo kubwa ambalo tulianza nalo ni kutoa elimu kwa umma kuhusu maradhi hayo pamoja na kuhamaisha wananchi kufanya mazoezi.

Swali: Tumbaku imetajwa kuwa kichocheo kikuu cha maradhi yasiyoambukiza, Wizara ya afya inafanya nini kuhakikisha matumizi haya yanakoma?

Jibu: Tanzania ni mwanachama wa WHO, pia tumesaini na kuukubali mkataba na kupunguza matumizi ya tumbaku (Tobacco Control) duniani ya mwaka 2007.

Sheria hii nikiri kwamba imepitwa na wakati na kuna maeneo hayajawa vizuri katika utekelezaji wa sheria.

Kuna maeneo tumefanikiwa hasa ya viwanja vya ndege, ambako kuna mabangoi yaliyobandikwa na yanaonya wavutaji waache kuvuta sigara ovyo, na kweli hawavuti.

Katika hili naweza kusema kuwa tumepiga hatua kwa sababu tayari kuna maeneo yametengwa maalumu kwa ajili ya wavuta sigara.

Changamto inakuja katika baadhi ya maeneo ya wazi, bado hatujafanikiwa, sheria inasema watu wasivute maeneo ya wazi lakini nani ambaye anasimamia ni polisi au ofisa afya.

Hapa sheria haijakaa sawa, ndiyo maana kabla mimi sijaingia kulikuwa na jitihada za kufanya marekebisho ya sheria ya tumbaku kusudi tupate sheria mpya ambayo itaianisha kila kitu kwa utekelezaji na uwajibikaji.

Lakini pia tukubaliane kuwa ile mpya ambayo ilikuwa inaelekezwa, ilizungumzia masuala ya kudhibiti kilimo cha tumbaku, sasa ukimwambia mwananchi wa Tabora Urambo kule vijijini asilime tumbaku na wao ndiyo sehemu ya kuongeza kipato chao, hawakuelewi.

Tunachojitahidi kukizungumza ndani ya Serikali na kwa wenzetu wa sekta ya kilimo ni kuja na mazao mbadala ambayo yataweza kuwasaidia wananchi kuongeza kipato chao, lakini pia hayatakuwa na athari katika kipato chao na maisha yao ya baadaye.

Swali: Mbali na hayo bado tumbaku itaendelea kutumika. Jitihada gani zaidi zinafanywa?

Jibu: Nafurahi sana na ndani ya wiki mbili zilizopita kimeitishwa kikao na Ofisi ya Waziri Mkuu kukubaliana sasa ni jinsi gani tunaweza kuwa na msimamo wa pamoja wa nchi na Serikali katika kudhibiti matumizi ya tumbaku.

Lakini kwa upande wetu Wizara ya Afya, tumesema wakati tunaendelea kubunga bongo kupata sheria nzuri zaidi ya kudhibiti matumizi ya tumbako, hatutazuia wala kupinga kilimo cha tumbaku kwa sasa.

Tutaelimisha wananchi juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku, hiyo ndiyo kazi kubwa ambayo tunaifanya, Wizara ya Kilimo wataendelea na kilimo sisi tutaelimisha.

Swali: Ili kuepuka kutumia gharama kubwa katika kutibu maradhi haya, Serikali inafanya nini kwenye kukinga?

Jibu: Hata katika mkutano wa 65 wa mawaziri wa afya wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika, tulijadili kwamba kisababishi kikubwa cha maradhi yasiyoambukiza ni matumizi ya tumbaku na pombe kupita kiasi, lakini pia suala la mtindo wa maisha, wengi hawafanyi mazoezi, mtu anatoka kilomita moja au mbili anataka kupanda daladala, bodaboda. Pia shida ya ulaji usiofaa.

Hivyo ni lazima kila nchi ichukue hatua ya kudhibiti kwa kutoa elimu kwa umma ya kuepukana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya, unaonyesha asilimia 97 ya Watanzania waliohojiwa iwapo wanakula mbogamboga na matunda zaidi ya mara tano kwa siku, asilimia 2.5 tu ndiyo walisema wanakula wengi hawali lakini wataalamu wanaagiza hivyo.

Swali: Upo utafiti uliofanywa hivi karibuni unaoonyesha hali halisi ya ongezeko la maradhi haya yasiyoambukiza?

Jibu: Utafiti rasmi ulifanyika mwaka 2012 takribani miaka sita sasa, lakini ukiangalia idadi ya wagonjwa ambao wanafika katika vituo vya kutoa huduma za afya inaongezeka.

Swali: Mwelekeo sasa ni upi?

Jibu: Sisi tumejipanga katika maeneo makubwa matatu; eneo la kwanza ni katika kukinga, pili ni kugundua mapema na eneo la tatu ni kuhakikisha tunapata matibabu.

Swali: Kuna kiasi cha fedha WHO ilipendekeza kitengwe kwa kila Mtanzania kupambana na NCDs, je fedha hizo zinatosha au hazitoshi na je, Serikali inaweka mikakati gani kuhakikisha inafikia lengo?

Jibu: Sisi tunachopata ni lile fungu kutoka Serikali Kuu. Lakini ni kweli tukichukulia nchi ya Afrika Kusini sukari inatozwa kodi sababu ni moja ya kichocheo cha maradhi yasiyoambukiza fedha inayopatikana pale inachangia gharama za matibabu kwa wagonjwa wa kisukari.

Lakini kwenye matumizi ya pombe na sigara, sambamba na kodi zinazotozwa humo kuna nchi wenzetu wameenda mbali, kuna kodi zingine za nyongeza ambazo zinatoka katika vileo kunakuwa na mfuko wa afya ambao vyanzo vyake vinakuwa ni kodi kama hizo kwa ajili ya lengo la kugharamia matibabu ya maradhi yasiyoambukiza. Ila kwa sisi bado hatujafikia hatua hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz